Naibu Waziri amemuagiza Afisa Elimu Sekondari mkoa wa Kigoma na Halmashauri ya wilaya ya Kigoma kutoa maelezo ya maandishi kwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Adolf Nduguru ya kwanini walitoa taarifa ya kukamilika kwa ujenzi wa shule ya sekondari ya Nkungwe ilihali ikiwa bado haijakamilika.
Mhe. Ndejembi ametoa agizo hilo wakati wa ziara yake ya kukagua ujenzi wa shule za sekondari katika wilaya ya Kigoma ambapo ameeleza kutoridhishwa na ujenzi wa shule hiyo huku akimtaka Mkurugenzi wa Halmashauri kumchukulia pia hatua za kinidhamu Mhandisi wa halmashauri na Mhandisi anayesimamia mradi huo.
"Namuagiza Katibu Mkuu TAMISEMI, kwanza apokee maelezo ya maandishi kutoka kwa maafisa elimu hawa ya kwanini wametoa taarifa ambazo siyo sahihi, taarifa walizozileta kwa Ofisi ya Rais-TAMISEMI ni kwamba shule hii imekamilika jambo ambalo siyo kweli," amesema Ndejembi.
Aidha Ndejembi ameongeza kuwa, "Tumekagua ujenzi huu wote na tumejionea kwamba madarasa yenyewe bado hayajakamilika, milango haijafungwa, madawati hayajawekwa na hata vyoo vyenyewe bado havijakamilika, sasa kwa uzembe huu hatuwezi kukaa kimya lazima tuchukue hatua za kinidhamu kwa wote waliohusika,".
0 Comments