Serikali mkoani Tabora imeziagiza halmashauri zote saba za mkoa huo kufuta tozo wanazolipishwa wananchi katika kupata huduma za vyoo maeneo yenye mikusanyiko kama vituo vya mabasi na masokoni ili huduma hiyo iweze kutolewa bure ikiwa ni moja ya mikakati ya kuthibiti maambukizi ya mlipuko wa kipindupindu kinachodaiwa kubisha hodi mikoa jirani inayopakana na Tabora.
Akizungumza na wadau katika kikao cha dharura alichoitisha Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Balozi Dkt..Batilda Buriani amesema ingawa Tabora bado haujafikiwa na mlipuko huo wa kipindupindu ni vema kuweka mikakati ambayo itasaidia kudhibiti ugonjwa huo.
Dkt.Batilda alitumia kikao hicho pia kuwa tayari wakati wowote kukabiliana na janga hilo sambamba na kumuagiza mganga mkuu kuhakikisha anafuatilia wizarani vifaa muhimu vinavyotumika kuwahudumia wagonjwa wa kipindupindu.
Wakati mikakati hiyo ikifanyika hali ya Soko Kuu la Tabora na vyoo vya kulipia vilivyopo vinadaiwa kutokuwa katika mazingira mazuri na uchafu umezagaa na kusababisha malalamiko kutoka kwa baadhi ya wananchi.
0 Comments