
SERIKALI imesaini mikataba ya zaidi ya Sh. bilioni 200 kwa ajili ya Mradi wa Uboreshaji wa Huduma ya Majisafi na Usafi wa Mazingira katika Manispaa ya Morogoro na kwamba wakandarasi wameshaanza kazi.
Hayo yamesemwa Novemba 26, 2026 na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, wakati akitoa taarifa mbele ya Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, kuhusu hali ya upatikanaji wa maji kwenye Manispaa hiyo katika mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Jamhuri, Morogoro Mjini.
Mradi huo unahusisha uboreshaji wa Bwawa la Mindu, ujenzi wa mtambo mpya wa kutibu maji wa Mafiga, matanki ya kuhifadhi maji pamoja na upanuzi wa mtandao wa mabomba ya kusambaza maji katika Manispaa ya Morogoro.
“Mahitaji ya maji katika Manispaa ya Morogoro ni lita milioni 89 kwa siku, wakati uzalishaji ni lita milioni 40 na hushuka hadi milioni 30 wakati wa kiangazi, hali inayosababisha upungufu wa lita milioni 59 kwa siku,” alisema Waziri wa Maji baada ya Waziri Mkuu kupokea malalamiko ya shida ya maji kutoka kwa wakazi waliohudhuria mkutano huo.
Akielezea kuhusu fidia kwa wananchi waliopisha mradi, Waziri Aweso alisema fedha za awamu ya kwanza zimeshatolewa na amemwelekeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji ahakikishe fedha zinapatikana haraka ili kukamilisha malipo kwa wananchi ambao bado hawajalipwa.
Akifafanua suala hilo, Dkt. Mwigulu Nchemba alisema imetosha kwa wananchi wa Morogoro kuendelea kukabiliwa na tatizo la upungufu wa maji, huku akiitaka Wizara ya Maji ihakikishe wakandarasi wanaotekeleza mradi mkubwa wa maji mkoani humo wanafanya kazi usiku na mchana ili kuharakisha ujenzi wake.
Alisema haikubaliki Mkoa wa Morogoro kuendelea kuwa na mgawo wa maji wakati ni miongoni mwa vyanzo muhimu vya maji yanayosambazwa katika mikoa ya Pwani na Dar es Salaam. “Imetosha sasa kuendelea kuona Mkoa wa Morogoro ukipata shida ya maji na wananchi wake wakipata shida ya maji,” amesema.
Dkt. Mwigulu amesema Serikali inataka kuona mradi huo unatekelezwa kwa kasi ili wananchi wapate huduma ya uhakika badala ya kuendelea kukabiliwa na mgawo wa maji. “Mheshimiwa Waziri, wasisitizie watu wanaotekeleza mradi huo wafanye kazi usiku na mchana tumalize ujenzi wa miundombinu ili wananchi hawa wapate maji ya uhakika,” amesema.
Amesema Serikali imefanya mabadiliko ya sheria ili fedha za miradi ya maji, barabara na umeme vijijini ziweze kwenda moja kwa moja kwenye mifuko inayohusika, hatua inayolenga kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Amesisitiza kuwa mabadiliko hayo yanapaswa kuleta matokeo yanayoonekana kwa wananchi kupitia kukamilika kwa miradi na kuimarika kwa huduma muhimu.












0 Comments