Meneja wa Uhusiano na Mawasiliano wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Hamis Dambaya, akiwasilisha mada kuhusu vivutio vya utalii vya Ngorongoro na juhudi za kutangaza utalii wa ndani, wakati wa Kongamano la Mwaka la Tathmini ya Huduma za Habari na Mawasiliano Vijijini nchini Tanzania, lililoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Vijijini Tanzania (RUJAT), sambamba na Mkutano Mkuu wa Mwaka wa chama hicho, jijini Dodoma, Oktoba 31, 2026.
Picha na Kadama Malunde
Meneja wa Uhusiano na Mawasiliano wa Ngorongoro, Hamis Dambaya, akiwasilisha mada wakati wa Kongamano na Mkutano Mkuu wa Mwaka wa RUJAT jijini Dodoma, Oktoba 31, 2026.
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Katika kuimarisha juhudi za kutangaza utalii wa ndani na kuongeza ushiriki wa Watanzania katika sekta ya utalii, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) imeingia katika ushirikiano na Chama cha Waandishi wa Habari Vijijini Tanzania (RUJAT), kwa lengo la kuwajengea waandishi uelewa kuhusu vivutio, fursa na urithi wa kipekee unaopatikana katika Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.
Kupitia ushirikiano huo, waandishi wa habari wanatarajiwa kuwa mabalozi wa utalii kwa kutumia vyombo vyao vya habari, majukwaa ya kidijitali na taaluma yao kufikisha taarifa sahihi kuhusu vivutio vya Ngorongoro kwa wananchi wa makundi mbalimbali, hususan wanaoishi vijijini na pembezoni mwa miji ambao huenda hawajapata fursa ya kutambua utajiri wa vivutio vya utalii nchini.
Akizungumza Oktoba 31,2026 wakati akiwasilisha mada katika Kongamano la Mwaka la Tathmini ya Huduma za Habari na Mawasiliano Vijijini nchini Tanzania, lililoandaliwa na RUJAT, sambamba na Mkutano Mkuu wa Mwaka wa chama hicho jijini Dodoma, Meneja wa Uhusiano na Mawasiliano wa Ngorongoro, Hamis Dambaya, amesema eneo la Hifadhi ya Ngorongoro hupokea wastani wa watalii zaidi ya milioni moja kwa mwaka, ambapo takribani asilimia 30 ni watalii wa ndani na asilimia 70 ni watalii kutoka nje ya nchi.
Dambaya amesema Ngorongoro inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali, wakiwemo waandishi wa habari na wadau wa sekta ya utalii, katika kutangaza bidhaa za utalii zinazopatikana katika eneo hilo ili kuwafikia Watanzania wengi zaidi na kuwahamasisha kutembelea vivutio vya ndani.
Amesema ushirikiano na RUJAT ni fursa muhimu ya kutumia nguvu ya vyombo vya habari katika kuelimisha jamii, kuongeza uelewa wa utalii wa ndani na kuifanya Ngorongoro ijulikane zaidi kwa wananchi wa maeneo mbalimbali nchini.
Kwa upande wake, Afisa Utalii wa Ngorongoro, Hillary Kimaro, amesema Ngorongoro ni kitovu cha maajabu mengi duniani, ikiwa na kaulimbiu ya Destination of Many Wonders, kutokana na kuwa na utajiri wa kipekee wa maliasili, wanyamapori, maeneo ya kihistoria, urithi wa utamaduni na mandhari ya asili.
Afisa Utalii wa Ngorongoro, Hillary Kimaro
Kimaro amesema Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro linatoa fursa ya kushuhudia matukio mbalimbali ya kipekee ya kiasili, ikiwemo kuzaliwa kwa ndama wa nyumbu katika kipindi cha uzazi kabla ya kuanza kwa safari ya uhamaji wa makundi ya nyumbu.
Ameeleza kuwa vivutio hivyo vinaifanya Ngorongoro kuwa eneo lenye uzoefu mpana wa utalii, linalounganisha uhifadhi wa mazingira, historia, utamaduni na maisha ya wanyamapori katika eneo moja.
Naye Afisa Uhusiano Mkuu wa Ngorongoro, Kassim Nyaki, amesema Ngorongoro ni zaidi ya hifadhi ya wanyamapori kutokana na kuwa na hadhi tatu za kimataifa zinazotambuliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), pamoja na mfumo wa matumizi mseto ya ardhi unaowezesha shughuli za uhifadhi wa wanyamapori na shughuli za binadamu kuendelea katika eneo moja kwa kuzingatia taratibu za uhifadhi.
Afisa Uhusiano Mkuu wa Ngorongoro, Kassim Nyaki.
Nyaki amesema wageni wanaotembelea Ngorongoro hupata fursa ya kushiriki shughuli mbalimbali za utalii, zikiwemo utalii wa picha, matembezi na kupanda milima, safari za puto kwa ajili ya kutazama wanyamapori, kutembelea maeneo ya kihistoria na kujifunza urithi wa utamaduni.
Shughuli nyingine ni kuendesha baiskeli, kupanda farasi, kutazama ndege na kujionea mandhari ya kipekee ya asili, hali inayofanya Ngorongoro kuwa eneo linalotoa uzoefu tofauti wa utalii kwa wageni wa makundi mbalimbali.
Akizungumzia ushirikiano huo, Mwenyekiti wa RUJAT, Neville Meena, amesema chama hicho kinatambua nafasi kubwa ya waandishi wa habari katika kukuza utalii wa ndani, kuelimisha jamii na kutangaza fursa mbalimbali za maendeleo zinazopatikana nchini.

Mwenyekiti wa RUJAT, Neville Meena
Amesema ushirikiano na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ni fursa muhimu kwa waandishi wa habari za vijijini kupata maarifa sahihi kuhusu vivutio vya utalii, ili waweze kuvitangaza kwa wananchi kupitia vyombo vyao vya habari na majukwaa ya kidijitali.
Meena amesema RUJAT itaendelea kuhamasisha wanachama wake kuandika habari za kiutalii zenye ubunifu na mvuto, zitakazoonesha uzuri wa vivutio vya Tanzania, umuhimu wa uhifadhi na mchango wa utalii katika uchumi wa wananchi.
Ameongeza kuwa chama hicho kinaamini kuwa utalii haupaswi kutangazwa katika majiji makubwa pekee, bali taarifa zake zinapaswa kuwafikia wananchi wa vijijini ambao pia ni sehemu muhimu ya wadau wa sekta hiyo.



















0 Comments