Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Florent Kyombo, akizungumza wakati kamati hiyo ilipotembelea kuona na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo Manispaa ya Kahama, ikiwemo jengo la mama na mtoto pamoja na miradi ya Tactic.
Na
Neema Nkumbi - KAHAMA
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Florent Kyombo, ameielekeza
Manispaa ya Kahama kuhakikisha wafanyabiashara waliokuwa wakifanya shughuli zao
katika maeneo yanayojengwa upya, wanapewa kipaumbele katika masoko na vituo
vipya vya biashara.
Kyombo amesisitiza upangishaji wa bei
rafiki kwa wajasiriamali wa maeneo hao ili kutoa fursa kwa kila mmoja kufanya
shughuli za kujiingizia kipato.
Ametoa wito huo wakati wa ziara ya
kamati hiyo, iliyokagua miradi sita ya maendeleo katika Manispaa ya Kahama, akieleza
kuwa uwekezaji huo unapaswa kuwanufaisha wananchi waliokuwa wakitegemea maeneo
hayo kwa shughuli zao za kiuchumi.
Amesema “Kwa niaba ya Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan, miradi hii wakati inajengwa
kuna wananhi ambao walikuwa wanatoa huduma katika mazingira ambayo hayakuwa
katika kiwango kile kinachotakiwa, tunaomba viongozi wetu wa mkoa na wilaya,
tuhakikishe kwamba wale wenyeji wa maeneo yote wanapewa kipaumbele waweze
kuendeleza shughuli zao za kiuchumi.”
Sambamba na hilo amesisitza viongozi wa
Manispaa kusimamia gharama za upangishaji katika masoko na vituo vya mabasi
zinaendana na uwezo wa wafanyabiashara, ili miundombinu inayojengwa isiwatenge
wananchi ambao wamekuwa wakijipatia kipato kupitia shughuli hizo.
“Tunaendelea kuwasihi kuhusu bei za
kupangisha katika maeneo yetu ziwe bei rafiki kwa wananchi na wajasiriamali wote
wanaojitafutia kipato katika maeneo hayo.” Amesema Kyombo
Amesema wastani wa utekelezaji wa
miradi iliyokaguliwa umefikia asilimia 61, akiwataka viongozi, wakandarasi na
washauri elekezi kuongeza kasi ya kazi ili miradi ikamilike kwa wakati na
wananchi waanze kunufaika na huduma zake.
Amesema “Wananchi wanataka matokea,
wanataka kuona mirdi hii imekamilika, kwa hiyo tunaamini ndani ya kipindi hiki
cha mkataba mtamaliza, tukirudi wakati mwingine tukute miradi hii imekamilika.
TAMISEMI, naibu katibu mkuu tunaomba fedha tukamilishe”
TAMISEMI YAHIDI FEDHA ZA MIRADI
Naibu Katibu Mkuu wa TAMISEMI, John
Cheyo, amesema Serikali inaendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa
miradi ya maendeleo Kahama, akiwahakikishia wakandarasi kuwa fedha za kuwalipa
zipo.
“Naomba niseme tu kwamba fedha kwa ajili ya
kuwalipa wakandarasi wetu zipo, wakandarasi wanaofanya vizuri tupo nao sambamba
na tunatambua michango yao.” amesema Cheyo.
Kuhusu wafanyabiashara waliokuwa
katika eneo la soko kabla ya ujenzi, Cheyo amesema watapewa kipaumbele kurejea
katika maeneo hayo.
Amesema “Tutahakikisha wafanyabiashara
walioondoka katika maeneo yao kupisha ujenzi, watapewa kipaumbele kurejeshwa
kwenye maeneo yao. Kwa wengine sasa tutasimamia taratibu zingine ziendelee.”
Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga,
Pili Mnyema, amesema uwekezaji wa miradi ya kimkakati unaofanywa na Serikali mkoani
humo, unalenga kuinua uchumi wa Shinyanga, hivyo kwa kushirikiana na
halmashauri, watahakikisha utekelezaji wake unakuwa wa viwango vinavyotakiwa.
“Tumejipanga vizuri kuhakikisha kwamba
miradi yote inayoendelea inakamilika kwa wakati, kuna miradi mingi ya
kimkakati, kwa sababu dhamira na nia njema ya Mheshimiwa Rais ni kuhakikisha
mkoa wa Shinyanga unainuka kiuchumi, tupo tayari kuendelea kuisimamia.” Amesema
Mnyema.
NGAYIWA ATAKA WANANCHI WAPEWE NAFASI
Mbunge wa Kahama Mjini, Benjamin
Ngayiwa, amesema ugawaji wa maeneo haupaswi kufuata misingi ya vyama vya siasa,
bali kuzingatia maslahi ya wananchi na fursa za kiuchumi zinazotokana na uwekezaji
huo.
Aidha, ameitaka Serikali kuendelea
kutoa fedha kwa wakati ili mradi ukamilike haraka na wananchi waanze kunufaika
na huduma zinazotarajiwa.
MASINDI AWATAKA WAWEKEZAJI KUMIMINIKA KAHAMA
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Peter
Masindi, anayekaimu Wilaya ya Kahama, amewataka wawekezaji kutoka ndani na nje
ya Tanzania kutumia fursa za kiuchumi zilizopo Kahama, akieleza kuwa mazingira
ya kukuza biashara na uzalishaji ni rafiki.
Amesisitiza kuwa fursa za uwekezaji
Kahama zinapaswa kutumiwa kuongeza uzalishaji na kuchochea ukuaji wa uchumi,
huku akieleza kuwa maendeleo ya eneo hilo yanahitaji ushiriki wa Serikali,
sekta binafsi na wananchi wenyewe.
“Kahama milango ya kiuchumi imefunguliwa saa
24, watanzania njooni muwekeze Kahama, tunahitaji wawekezaji watakaochukua
fursa za kuzalisha kutoka maeneo mengine wazilete hapa.” Amesema Masindi.
Ameipongeza Serikali chini ya Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uwekezaji
unaofanyika, huku akiwataka wananchi kutunza miundombinu hiyo ili iendelee
kutoa huduma kwa muda mrefu.


































0 Comments