TANGAZO

TANGAZO

MATIBABU YA KIBINGWA SHINYANGA KUPUNGUZA GHARAMA ZA MATIBABU KWA WANANCHI

 

Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Nelson Mgaya


Na mwandishi wetu - Shinyanga 

Matibabu ya kibingwa ya pua,koo na sikio, yanatarajiwa kuwafikia zaidi ya wakazi elfu mbili kutoka Mkoa wa Shinyanga na maeneo ya jirani ambao watanufaika na huduma hizo  zilizoanza kutolewa  katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa huo.

Kuanza kwa huduma hiyo leo jumatatu Januari 5,2026 ni sehemu ya juhudi za Serikali za kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi ili kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda Mikoa mingine na kuongeza upatikanaji wa matibabu ya kitaalamu ndani ya Mkoa.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa huduma hizo, Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Nelson Mgaya, amesema kumekuwepo na ongezeko la magonjwa ya koo kwa watoto wadogo pamoja na changamoto ya usikivu hafifu kwa watu wazima, hatua ambayo inaashiria kuwepo kwa tatizo kubwa la kiafya katika jamii.

Dkt. Mgaya amesema kuanza kwa kliniki hiyo kutawawezesha wananchi kupata uchunguzi wa mapema, matibabu sahihi pamoja na ushauri wa kitaalamu, huku akiwataka wakazi wa Shinyanga na mikoa ya jirani kujitokeza kwa wingi kutumia huduma hizo.

Naye Mkuu wa Idara ya Upasuaji katika hospitali hiyo, DktGeofrey Mboye, amesema hospitali imejipanga kikamilifu kwa kuwa na wataalamu wa kutosha pamoja na vifaa tiba muhimu ili kuhakikisha huduma za pua, koo na masikio zinatolewa kwa ufanisi na kwa usalama.

Baadhi ya wananchi walioanza kunufaika na huduma hizo, akiwemo Magreth Nyange, wameishukuru Serikali kwa kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi, ambapo wameeleza hatua hiyo itapunguza gharama na usumbufu wa kusafiri umbali mrefu kufuata matibabu katika mikoa mingine

Post a Comment

0 Comments