TANGAZO

TANGAZO

WAZIRI MKUU MAJALIWA AZINDUA RASMI TUZO ZA UTALII NA UHIFADHI


Na mwandishi wetu, Arusha

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezindua rasmi tuzo za uhifadhi na utalii na kusisitiza kuwa Serikali itendelea kubuni mikakati ya kuimarisha sekta ya Maliasili na Utalii kwa kuwa sekta hiyo ni nguzo muhimu ya uchumi wa Taifa.


Amesema hayo Desemba 20, 2024 alipozindua Tuzo za Uhifadhi na Utalii katika Ukumbi wa Hoteli ya Mt. Meru jijini Arusha. Tuzo hizo zina lengo la kuchochea ushindani kati ya wadau wa sekta ya maliasili na utalii nchini.

Amesema kuwa Sekta ya maliasili na utalii ni chanzo kikubwa cha mapato ya taifa kwa kuwa inahusisha shughuli nyingi za kiuchumi.

“Sekta hii peke yake inachangia asilimia 21.5 katika pato ghafi la Taifa ambapo asilimia 17.2 ni utalii, asilimia 4.3 ni misitu na nyuki” amesema Mhe. Majaliwa.

Aidha, amefafanua kuwa Sekta hiyo inachangia asilimia 30.9 ya mapato ya fedha za kigeni ambapo asilimia 25 yanatokana na utalii, asilimia 5.9misitu na nyuki.
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa juhudi za dhati na maono makubwa ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuiendeleza Sekta ya Maliasili na Utalii yamesaidia kuongeza idadi ya watalii wa kimataifa kwa asilimia 96 kutoka watalii 922,692 mwaka 2021 hadi watalii 1,808,205 mwaka 2023;

“Jitihada za Rais wetu Dkt. Samia zimesaidia pia kuongezeka kwa mapato yatokanayo na Utalii wa Kimataifa kwa asilimia 68.2 kutoka dola za Marekani bilioni 2.0 mwaka 2021 hadi bilioni 3.4 mwaka 2023”.

Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa ameiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kuhakikisha inaweka vigezo vya wazi na vinavyojulikana vya uteuzi na upokeaji wa tuzo.

“Vigezo hivyo, pamoja na mambo mengine viwe vinavyozingatia ubora katika uhifadhi wa mazingira, huduma za utalii, usimamizi wa hifadhi za wanyama, na uendelezaji wa maeneo ya utalii” amesisitiza Mhe. Majaliwa.

Naye, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Balozi Dkt. Pindi Chana (Mb)amempongeza Rais Dkt. Samia kwa namna anavyojitoa katika kuhakikisha Sekta ya Maliasili na Utalii inaendelea kukua kwa kasi.

Ameongeza kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii imekuwa na mikakati mbalimbali ya kuimarisha uhifadhi na kuendeleza utalii ikiwemo kutumia teknolojia mbalimbali pamoja kuendeleza Programu ya Tanzania – the Royal Tour na kuibua mazao mapya ya utalii ili kuongeza idadi ya watalii na mapato yatokanayo na shughuli za utalii.










Post a Comment

0 Comments