Mwenyekiti wa usalama barabarani mkoa wa Simiyu Amos Kadonya
akikabidhi moja ya zawadi za sikukuu kwa wenye uhitaji Nyandekwa - Kahama,
ikiwa ni sehemu ya kurejesha shukrani katika eneo alipozaliwa.
Mwenyekiti wa usalama barabarani mkoa wa Simiyu Amos Kadonya akikabidhi zawadi za sikukuu kwa mmoja wa wenye uhitaji.
KAHAMA.
Mwenyekiti wa usalama barabarani mkoa wa Simiyu ambaye pia ni mjumbe wa mkutano mkuu wa CCM manispaa ya Kahama Amos Kadonya, amewakarimu wananchi zaidi ya 260 wenye uhitaji wakiwemo wazee, katika kata ya Nyandekwa manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga, kwa lengo la kuwawezesha kusherehekea vyema sikukuu za mwisho wa mwaka.
Kadonya
ametoa zawadi hizo Disemba 30/2024 ikiwa pia ni sehemu ya shukrani kwa wananchi
hao wa kata ya Nyandekwa alipozaliwa na kusoma masomo yake ya awali, ambapo
amegawa sukari, mchele pamoja na unga wa ngano.
Katika
hafla hiyo iliyofanyika katika Kijiji cha Nyandekwa kata ya Nyandekwa, manispaa
ya Kahama mkoani Shinyanga, wananchi wa Kijiji hicho wameeleza kukatishwa tamaa
ya kuendelea kuchangia miradi ya maendeleo katika eneo lao, kwa madai ya
Halmashauri kushindwa kamalizia kwa wakati majengo waliyoyaanzisha kwa nguvu
zao.
Clemensia
Mbago ni mkazi wa Nyandekwa Kahama amesema kukosekana kwa kituo cha afya katika
kata yao kunaathiri juhudi za serikali katika kuhamasisha na kuhakikisha huduma
bora ya baba, mama na mtoto, ikiwemo akina mama kujifungulia katika vituo vya
kutolea huduma za afya ili kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.
“Yaani
sasa hivi tuna miaka mitano tumeshamaliza kujenga, lakini serikali hakuna
kinachoendelea, tatizo tunalolipata ni akina mama wakati wa kujifungua maana
kuipata huduma hii ni km 3 hadi 4, hivyo inapelekea kuumiza mtoto au wote
kufariki kabisa” Alisema Clemensia
Mkazi
mwingine wa Nyandekwa Magreth Makoye, yeye akaeleza kuwa linapotokea suala la
msiba wanapata adha kubwa ya kusafirisha mwili wa mpendwa wao kutokana na
umbali wa hospitali na hivyo gharama kuwa kubwa.
“Kwa
bahati mbaya mtu amefariki, kumtoa Kahama inatuwia ugumu namna ya kuusafirisha
mwili wa marehemu gharama kubwa, lakini kama tukipata kituo cha afya hapahapa
inatuwia ni rahisi” Alisema Magreth
Mwenyekiti
wa Kijiji cha Nyandekwa Shadrack Bundala akieleza hatua zilizochukuliwa ili
kukamilisha ujenzi huo amesema kila alipojaribu kuhoji alijibiwa kuwa jengo
hilo tayari limeombewa fedha lakini bado hakuna kinachoendelea, huku akikiri
wananchi wake kupata adha kubwa kufuata huduma za afya katika vijiji maeneo ya
Jirani ikiwemo hospitali ya manispaa ya Kahama ambayo nayo ipo mbali na Kijiji
chao.
Bundala
amesema kutokana na hali hiyo wao kama viongozi wanakosa ujasiri wa kuendelea
kuchangia miradi mipya ya maendeleo jambo ambalo linaathiri utekelezaji wa
shughuli zao kwenye vijiji husika.
“Lakini
sijajua sijui ni siasa mbovu, kila ukiuliza mara unaambiwa limekuwa la rufaa
wakati bado ni boma tu, mara limeombwa fedha, kwa kweli mpaka tunavyosema hivi
sisi kama wananchi wa Kijiji cha Nyandekwa ambao ndio tuna msiba mkubwa, bado hatujajua hatima ya hilo jengo itakuwa ni
nini” Alisema Bundala
“Kwa
sababu mpaka tunavyokaa hivi wananchi hawa wanaendelea kuteseka kama
walivyosema, huduma wanapata mbali, kutoka hapa mpaka waende mjini au waende Lowa
na wakifika kule matibabu ni makubwa, mimi niiombe serikali itusikilize kero
hii iweze kutuingizia fedha kwa wakati ili sasa wananchi hawa waweze kupata
huduma zinazostahili” Aliongeza Bundala
Kadonya
ambaye pia ni mjumbe wa mkutano mkuu wa CCM manispaa ya Kahama, amewasihi
wananchi wa Nyandekwa kushikamana na na kushirikiana na viongozi wao waliowekwa
kikatiba ili kutatua changamoto zinazowakabili.
“Lakini
uongozi ambao upo madarakani ambao umechaguliwa kikatiba tuupe ushirikiano, la
kwanza tuwe na upendo, palipo na upendo kuna amani, palipo na upendo kuna Mungu,
palipo na upendo kuna mafanikio” Alisema Kadonya
Flora
Sangiwa ni kaimu mkurugenzi wa manispaa ya Kahama, ametoa wito kwa wawakilishi
wa serikali ngazi za chini kuhakikisha wanawaelimisha wananchi kuhusu mfumo
mpya ulioboreshwa unaowataka wananchi wanapoanzisha mradi kuukamilisha.
Sangiwa
amesema pamoja na hayo, tayari mradi wa kituo cha Afya Nyandekwa kipo kwenye utaratibu
wa kukamilishwa na katika mwaka ujao wa fedha halmashauri italimalizia ili
wananchi waanze kupatiwa huduma.
“Ni
wajibu wa wananchi na kupitia wawakilishi wetu pia kuwaeleza kuwa wanapoanzisha
hii miradi kupitia huu mfumo mpya ulioboreshwa walitakiwa wao wenyewe wawe
wamekamilisha” Alisema Sangiwa
“Lakini
pamoja na hayo, tayari boma hili lipo kwenye utaratibu wa kukamilishwa, na kwa
mwaka ujao wa fedha tunaweza tukalikamilisha boma hili, kwa sababu limekuwa ni
out-cry ya wananchi wa Nyandekwa.” Aliongeza
Mchakato
wa awali wa ujenzi wa kituo cha afya Nyadekwa ulianza rasmi mwaka 2015 kwa
nguvu za wananchi, ambapo mwaka 2020 hatua ya msingi ilikamilika na wananchi
kuendelea kujitolea kwa kujenga boma ambalo lilikamilika miaka mitano
iliyopita.
MWISHO.
0 Comments