TANGAZO

TANGAZO

RPC MAGOMI AZINDUA KITUO CHA POLISI ISAKA, WANANCHI WATAKIWA KUTOA TAARIFA ZA UHALIFU NA WAHALIFU


Na Steve Kanyefu, Kahama


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi, amezindua Kituo cha Polisi Kata ya Isaka katika Halmashauri ya Msalala, huku akiwataka wananchi kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu ili kuimarisha ulinzi na usalama katika eneo hilo.


Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kituo hicho, leo octoba 2,2026, Kamanda Magomi amesema uwepo wa kituo hicho, kilichojengwa kwa ushirikiano wa wananchi, wadau mbalimbali na Serikali, utasaidia kuimarisha hali ya usalama kwa wakazi wa Isaka na maeneo jirani.

 

“Niwaombe wananchi, kukamilika kwa kituo hiki uwe ni mwanzo wa ushirikiano mkubwa wa kuimarisha hali ya usalama kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu.”

 

Kamanda Magomi pia amewataka askari watakaopangiwa kufanya kazi katika kituo hicho kutekeleza majukumu yao kwa weledi na kuhakikisha wananchi wanaofika kupata huduma wanatendewa haki.

 

“Tumejifunza upolisi, tunatakiwa tutende haki kwa wananchi wanaokuja kupokea huduma kwetu,”

 

Katika uzinduzi huo, ACP Dkt. Method Mtana, aliyemwakilisha Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Tanzania, IGP Camilius Wambura, aliwapongeza wananchi kwa kushiriki katika ujenzi wa kituo hicho na kuwataka kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi pamoja na sungusungu katika kulinda kituo na miundombinu yake.

 

“Mkuu wa Jeshi letu anawashukuru sana wananchi kwa kuanzisha ujenzi wa kituo hiki. Niwaase wananchi kwa kushirikiana na sungusungu mvilinde vituo hivi kwa hali na mali.”

 

Mbunge wa Jimbo la Msalala, Mabula Magangila, amesema kuimarika kwa ulinzi na usalama kutasaidia kuchochea ukuaji wa uchumi katika eneo hilo, hasa kutokana na ongezeko linalotarajiwa la magari makubwa yanayofika katika eneo hilo.

 

“Miaka mitatu ijayo, maroli yatakayoingia hapa tunatarajia sio chini ya 600 kwa siku. Kwa maana hiyo hatutaki kuwepo na viashiria vya wizi katika eneo hili, ulinzi na usalama umeimarishwa.”

 

Kwa mujibu wa Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Kipolisi Msalala (OCD), Yahya Shabani, ujenzi wa kituo hicho umegharimu jumla ya Shilingi milioni 236, fedha zilizopatikana kupitia ushirikiano wa wananchi, wadau mbalimbali na Serikali.

 

Amebainisha kuwa Wananchi na wadau walichangia zaidi ya Shilingi milioni 26 katika awamu ya kwanza, huku awamu ya pili ikipokea Shilingi milioni 100 na awamu ya tatu Shilingi milioni 110 zilizotumika kukamilisha ujenzi wa kituo hicho.

 

Kukamilika na kuzinduliwa kwa kituo hicho kunatarajiwa kuongeza upatikanaji wa huduma za Polisi kwa wananchi wa Kata ya Isaka na maeneo ya jirani, pamoja na kuimarisha ulinzi na usalama katika eneo hilo ambalo linaendelea kukua kwa kasi kiuchumi.












Post a Comment

0 Comments