Mbunge wa Kahama Mjini Benjamin Ngayiwa akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kijiji cha Isagehe, kata ya Isagehe, Manispaa ya Kahama, akisikiliza na kutatua kero za wananchi.
Video 👇
KAHAMA
Baadhi ya wananchi wa kata ya Isagehe, Manispaa ya Kahama, wameiomba serikali kuzingatia ushirikishwaji wa wananchi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kwenye maeneo yao kuepusha migogoro.
Wamesema wananchi kutoshirikishwa ipasavyo, huku wakitolea mfano wa ujenzi wa Bwawa la Umwagiliaji la Malenge, linalodaiwa kuathiri baadhi ya mashamba yao bila ridhaa yao kunaweza kusababisha maafa licha ya faida kubwa za miradi hiyo.
Wameyazungumza hayo kwenye mkutano wa hadhara wa mbunge wa Kahama Mjini Benjamin Ngayiwa, ulioanyika kata ya Isagehe, kusikiliza na kutatua kero za wananchi.
Wamesema hawapingi uwepo wa bwawa hilo, kutokana na umuhimu wake kwao, lakini wanataka utaratibu wa kuwashirikisha wananchi na kuwafahamisha kuhusu mradi uzingatiwe kabla ya utekelezaji wa mradi husika.
Mmoja wa wananchi hao Shija Nalimi amesema endapo wananchi wangeshirikishwa kuhusu mradi pamoja na maeneo ambayo yangeathiriwa, kero zilizopo sasa zingeweza kuepukika.
Amesema kwa upande wake, eneo la kilimo lenye takribani hekari 30 zimeathiriwa na bwawa hilo, huku akieleza kuwa familia yake imepoteza sehemu ya kilimo walipokuwa wakilima mazao ya chakula.
“Wanapotaka kuleta mradi, wananchi tushirikiswe ili tutoe maoni ya kurudhika ama kutoridhika na mradi, itasaidia kuondoa kero kama zilizopo sasa. Mbunge aliyetoka aliliona hili na analifahamu,”
Amesema wananchi kutoka maeneo yanayozunguka bwawa la Malenge, wanahitaji kupewa nafasi ya kushiriki na kunufaika na fursa zinazotokana na miradi ya kilimo, kutokana na baadhi yao kufanya kilimo bila miundombinu ya umwagiliaji.
Nae Yohana Athuman mkazi wa kijiji cha Isagehe amesema “Bwawa hili linawanufaisha zaidi wananchi wa Malenge na baadhi ya maeneo huku, lakini mimi ninachoomba kama itawezekana tuletewe trekta tuchimbe mabwawa binafsi”
Afisa Mahusiano mgodi wa Buzwagi Yunia Wang’oya amesema “Mradi huu tulikuwa tunafanya kwa kushirikiana na Halmashauri, ambapo kuhusu uhamaishaji lilikuwa ni jukumu la idara ya kilimo na idara ya maendeleo ya jamii.”
Mbunge wa Kahama Mjini Benjamin Ngayiwa amesema kuwa suala la wananchi ambao mashamba yao yameathiriwa na bwawa linahitaji kushughulikiwa kwa utaratibu unaotambua umuhimu wa bwawa hilo kwa wananchi.
Ameielekeza kamati ya maendeleo ya kata ya Isagehe (WDC) itakapokutana ifanye tathmini kuwatambua wananchi ambao mashamba yao yameathiriwa na bwawa hilo kisha iundwe kamati iakayoona namna ya kuwafidia wananchi ao.
Amesema “Fanyeni tathmini tena kwamba ni watu wangapi ambao mashamba yao yamemezwa na bwawa, ni eneo kiasi gani, ili iundwe kamati itakayoona hawa watu wanafidiwaje.”
Amesema hatua ya msingi ni wataalamu kufika katika maeneo yaliyoathiriwa, kufanya tathmini na kubaini wananchi ambao wanastahili kupata fidia kwa mujibu wa taratibu.







0 Comments