Mbunge wa jimbo la Kahama Mjini Benjamin Ngayiwa akigawa vyeti kwa wahitimu wa darasa la saba shule y msingi Shunu, katika mahafali ya 18 ya shule hiyo iliyopo katika Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga.
Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Shunu, Mwalimu Edward Kinungu (kulia), akiwa na mgeni rasmi katika mahafali ya 18 ya shule ya msingi Shunu ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Kahama Mjini Benjamin Ngayiwa (Kushoto).
wahitimu wa darasa la saba shule ya msingi Shunu, wakiwa katika picha ya pamoja.
Neema Nkumbi, Kahama.
Mbunge wa Jimbo la Kahama Mjini, Benjamin Ngayiwa, ameahidi kuipatia Shule ya Msingi Shunu mashine mpya ya fotokopi kwa ajili ya kurahisisha uandaaji wa mitihani na mazoezi ya wanafunzi, huku akiahidi kufuatilia changamoto za miundombinu chakavu, upungufu wa matundu ya vyoo na walimu katika shule hiyo.
Ngayiwa ametoa ahadi hiyo wakati akijibu risala ya wahitimu wa mahafali ya 18 ya Shule ya Msingi Shunu, iliyopo Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga, ambapo wanafunzi wamewasilisha changamoto mbalimbali zinazokabili shule hiyo.
Katika risala hiyo iliyosomwa na Yuster Sabato, ameeleza kuwa shule hiyo inakabiliwa na miundombinu chakavu inayohitaji ukarabati, upungufu wa matundu ya vyoo vya wanafunzi pamoja na kutokuwa na vyoo vya walimu, hali inayohitaji hatua za kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.
Pia, ameomba kupatiwa vifaa vya teknolojia ikiwemo kompyuta, projekta na mashine ya fotokopi ili kurahisisha ufundishaji, ujifunzaji na upimaji wa maendeleo ya wanafunzi kupitia majaribio na mitihani ya mara kwa mara.
Akijibu changamoto hiyo, Ngayiwa amesema suala la mashine ya fotokopi si mara ya kwanza kulisikia kutoka shuleni hapo, akieleza kuwa katika ziara yake ya awali alikabidhiwa changamoto hiyo na baadaye mashine ilipatikana, lakini baadhi ya nakala zilizokuwa zikitolewa hazikuwa katika ubora unaotakiwa.
“Nalichukua tena kwa mara ya pili, na sasa tunaenda kuleta mashine mpya, Tutatafuta mashine nzuri na kuileta shuleni ili walimu waweze kuendelea na kazi zao,” amesema Ngayiwa.
Kuhusu upungufu wa matundu ya vyoo, mbunge huyo amesema atafuatilia suala hilo ili kuhakikisha shule hiyo inapata vyoo vya kutosha kwa wanafunzi na walimu, akisisitiza kuwa mazingira bora ni muhimu kwa ustawi wa jamii ya shule.
Amesema pia atafuatilia suala la upungufu wa walimu, akieleza kuwa baadhi ya walimu wamehamishwa na wengine kustaafu bila kupatikana kwa walimu wa kuziba nafasi zao, jambo linaloweza kuongeza mzigo wa kazi kwa walimu waliopo.
Katika hatua nyingine, Ngayiwa amewataka wazazi na wadau wa elimu kushirikiana katika kuhakikisha wanafunzi wanapata chakula shuleni, akisisitiza kuwa lishe bora ni sehemu muhimu ya kuwawezesha wanafunzi kuzingatia masomo na kufanya vizuri kitaaluma.
Hata hivyo, amesisitiza kuwa michango ya shule inapaswa kujadiliwa na kukubaliwa na wazazi kupitia vikao halali vya shule, akionya dhidi ya kuanzishwa kwa michango isiyofahamika au isiyopitishwa kwa utaratibu unaotakiwa.
Akizungumzia maendeleo ya kitaaluma, Ngayiwa amewapongeza walimu, kamati ya shule na wazazi kwa juhudi zao katika kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu na kufikia hatua ya kuhitimu elimu ya msingi.
Kwa mujibu wa risala ya wahitimu, shule hiyo imekuwa ikipata matokeo ya ufaulu katika mitihani ya kitaifa, huku ikitajwa kuwa na kiwango cha ufaulu cha asilimia 83 mwaka 2021, asilimia 88 mwaka 2022, asilimia 97 mwaka 2023 na asilimia 99 mwaka 2024.
Mahafali hayo yamefanyika huku jumla ya wanafunzi 197 wakihitimu elimu ya msingi, kati ya wanafunzi 198 waliosajiliwa kufanya Mtihani wa Taifa wa Darasa la Saba, huku mwanafunzi mmoja, Happiness, akishindwa kufanya mtihani kutokana na changamoto ya ugonjwa.
Ngayiwa amesema atafuatilia hali ya mwanafunzi huyo kwa kushirikiana na mzazi au mlezi wake, akieleza matumaini yake kuwa atapata nafuu na kurejea masomoni ili aweze kufanya mtihani katika mwaka unaofuata.
Mbunge huyo pia amezungumzia changamoto za barabara katika maeneo mbalimbali ya Jimbo la Kahama Mjini, akieleza kuwa juhudi za kuboresha miundombinu hiyo zinaendelea. Kuhusu huduma ya maji katika eneo la Shunu, amesema tenki la maji limekamilika na maji yameanza kutoka.
Akihitimisha hotuba yake, Ngayiwa amewataka wahitimu kuendelea kusoma kwa bidii, kuzingatia nidhamu, kuheshimu wazazi na walezi wao pamoja na kutumia elimu waliyoipata kujenga maisha yao na kuchangia maendeleo ya jamii na Taifa.
TAZAMA PICHA 👇












































0 Comments