Meneja wa TARURA wilaya ya Kahama, Mhandisi Joseph Mkwizu, akisoma taarifa ya daraja la mto Ndalilo kwa kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru 2026, uliofika kulizindua tayari kwa matumizi na kuwaondolea adha ya kusombwa na maji wananchi wa maeneo hayo.
Mbunge wa jimbo la Msalala, Mabula Magangila, akizungumza wakati wa uzinduzi wa daraja la Ndalilo, lililopo kata ya Ikinda, halmashauri ya Msalala uliofanywa na mwenge wa Uhuru 2026.

Wakazi wa kijiji cha Ndalilo, kata ya Ikinda, halmashauri ya Msalala, wilayani Kahama, mkoani Shinyanga, wameanza kunufaika na daraja jipya lililojengwa na serikali katika mto Ndalilo kwa gharama ya zaidi ya Shilingi milioni 400, hatua inayotarajiwa kuimarisha usalama na kurahisisha usafiri katika eneo hilo.
Kwa muda mrefu, wakazi hao walikabiliwa na changamoto ya kuvuka mto huo, hususani katika msimu wa mvua ambapo maji yaliongezeka na kusababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi pamoja na kuhatarisha shughuli zao za kila siku.
Meneja wa TARURA wilaya ya Kahama, Mhandisi Joseph Mkwizu, akizungumza wakati wa uzinduzi wa daraja hilo ulioanywa na mwenge wa uhuru, ameeleza hatua zilizochukuliwa na Serikali katika ujenzi wa daraja hilo pamoja na umuhimu wake kwa wakazi wa eneo hilo.
Baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Ndalilo, Maduhu Hangi na John Nkinga, wameeleza changamoto walizokuwa wakikabiliana nazo kabla ya kukamilika kwa daraja hilo, wakisema ujenzi wake umeondoa kero iliyodumu kwa muda mrefu.
Nae mbunge wa Msalala, Mabula Magangila, amepongeza juhudi za serikali katika kutekeleza mradi huo, akieleza kuwa daraja hilo ni sehemu ya maboresho yanayolenga kuboresha maisha ya wananchi.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Wazo Michael Mwang’onda, amesisitiza umuhimu wa wananchi kulitunza daraja hilo ili liweze kudumu na kuendelea kutoa huduma kwa wananchi kwa muda mrefu.


0 Comments