Na Mwandishi wetu
Kilwa, Lindi. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano Kazini), Deus Sangu, amewahimiza vijana mkoani Lindi kujiandaa kutumia fursa za ajira, biashara na uwekezaji zitakazotokana na kukamilika kwa Mradi wa Kimkakati wa Bandari ya Uvuvi ya Kilwa Masoko.
Akizungumza baada ya kukagua mradi huo, Sangu amesema bandari hiyo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kukuza uchumi wa buluu na kuongeza nafasi za ajira kwa Watanzania, hususan vijana.
"Bandari hii inatarajiwa kuzalisha zaidi ya ajira 30,000. Vijana wanapaswa kujiandaa sasa ili wawe sehemu ya fursa zitakazotokana na mradi huu," amesema.
Amesema bandari hiyo inatarajiwa kuhudumia zaidi ya tani 60,000 za samaki kwa mwaka, hatua itakayoongeza shughuli za uvuvi, biashara na uchakataji wa mazao ya baharini.
Sangu amesema mradi huo pia unaunga mkono utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambayo inalenga kuongeza mchango wa sekta binafsi katika ukuaji wa uchumi na kuzalisha zaidi ya ajira milioni nane nchini.
Aidha, amesema Serikali inalenga kuongeza mchango wa sekta ya uvuvi katika Pato la Taifa kutoka asilimia 2.2 za sasa hadi kufikia asilimia 9.8 ifikapo mwaka 2050.
Akiwasilisha taarifa ya mradi, Msimamizi wa Mradi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mhandisi George Kwandu, amesema ujenzi wa Bandari ya Uvuvi ya Kilwa Masoko umekamilika kwa asilimia 100, huku Serikali ya Awamu ya Sita ikitoa Shilingi bilioni 225 kati ya gharama ya jumla ya Shilingi bilioni 280 za mradi huo.
Amesema wakati wa ujenzi mradi huo ulitoa ajira 1,270, huku ajira za moja kwa moja 300 zikitarajiwa wakati wa uendeshaji wa bandari na zaidi ya ajira 30,000 kunufaisha wananchi kupitia shughuli mbalimbali zitakazozunguka bandari hiyo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Mohamed Nyundo, amesema tayari wilaya imeanza kutoa elimu kwa vijana kuhusu fursa za kiuchumi zitakazotokana na bandari hiyo ili wawe tayari kunufaika mara shughuli zitakapoanza.
Naye Mbunge wa Kilwa Kusini, Hasnain Dewji, amesema bandari hiyo inatarajiwa kuvutia wawekezaji na wafanyabiashara wa sekta ya uvuvi kutoka ndani na nje ya Tanzania, akitaja nchi za Somalia, Kenya na Msumbiji kuwa miongoni mwa zilizokwisha kuonesha nia ya kuitumia.
Ameongeza kuwa mapato ya Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa yanatarajiwa kuongezeka kutoka takribani Shilingi bilioni 10 za sasa hadi kufikia Shilingi bilioni 25 baada ya bandari kuanza kufanya kazi kikamilifu.
Waziri Sangu yuko katika ziara ya kikazi ya siku tano mkoani Lindi kukagua miradi ya maendeleo na kuzungumza na wananchi kuhusu utekelezaji wa miradi ya Serikali.



0 Comments