TANGAZO

TANGAZO

DC NKINDA : TUWE DARAJA LA MAPENZI KATI YA WANANCHI NA SERIKALI




🎈KAHAMA.

Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Frank Nkinda, amewataka wenyeviti wa Serikali za Vijiji na Mitaa katika Halmashauri za Msalala, Ushetu na Manispaa ya Kahama kutambua dhamana kubwa waliyonayo katika kujenga uhusiano mzuri kati ya wananchi na Serikali kwa kusikiliza na kutatua kero zinazowakabili katika maeneo yao.


Nkinda ametoa kauli hiyo wakati wa kikao kazi na wenyeviti wa Serikali za Vijiji na Mitaa Wilaya ya Kahama, akisisitiza kuwa viongozi hao ndio waliopo karibu zaidi na wananchi, hivyo utendaji wao unaweza kuwa daraja la kujenga mapenzi na imani ya wananchi kwa Serikali au kuwa chanzo cha chuki na kupungua kwa imani hiyo.


Amesema moja ya changamoto zinazoendelea kuwaumiza wananchi ni migogoro ya ardhi pamoja na madai ya dhuluma, hali ambayo kwa kiasi kikubwa inaweza kupunguzwa iwapo viongozi na watumishi katika ngazi za vijiji, mitaa, kata na wilaya watasimamia ipasavyo majukumu waliyopewa.




"Viongozi wa Serikali za Mitaa na Vijiji, tumebeba dhamana kubwa ya kuwa daraja la mapenzi ya wananchi kwa Serikali yao au chuki kati ya wananchi dhidi ya Serikali," amesema Nkinda.


Ameeleza kuwa kuendelea kuibuka kwa migogoro na malalamiko kutoka kwa wananchi kunapaswa kuwafanya viongozi kujitathmini namna wanavyotekeleza wajibu wao, badala ya kusubiri matatizo yafike katika ngazi za juu ndipo hatua zichukuliwe.


Kwa mujibu wa Nkinda, baadhi ya wenyeviti kutofanya vikao na mikutano ya mara kwa mara ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi katika mitaa, vijiji na kata, kumechangia wananchi kukosa maeneo rasmi ya kueleza changamoto zao na hivyo kuamua kutumia mitandao ya kijamii kama sehemu ya kutoa malalamiko.




"Wajibu umekuwa tatizo, Wenyeviti kutokufanya vikao na mikutano ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi mitaani, vijijini na ngazi za kata ipasavyo, kumetoa mwanya kwa wananchi kupumua mitandaoni badala ya kupumua kupitia mikutano na vikao vya ngazi husika," amesema.


Aidha, DC Nkinda amewakumbusha viongozi hao kuwa nafasi walizonazo si za kudumu, hivyo wanapaswa kuzitumia kuwahudumia wananchi, kutetea maslahi ya taifa na kuijengea heshima Serikali badala ya kuweka mbele maslahi yao binafsi.


Amesisitiza kuwa madaraka waliyopewa viongozi ni kwa ajili ya kutumikia wananchi na si kutumikiwa, huku akiwataka kuongeza uwajibikaji na kuhakikisha huduma wanazotoa zinawafanya wananchi kuridhika na Serikali yao.




"Hakuna nafasi inayodumu chini ya jua, nafasi na vyeo vinapita. Tukachape kazi, tuiheshimishe Serikali ya CCM iliyotupa imani na tuhakikishe huduma tunazotoa zinawafurahisha wananchi tunaowaongoza," amesema Nkinda.


Pia amewataka viongozi kutambua kuwa uongozi ni dhamana ambayo pamoja na kuwajibika mbele ya wananchi, kila mmoja anapaswa kutambua wajibu wake mbele ya Mungu kwa nafasi na mamlaka aliyopewa.


Kikao hicho kimewakutanisha wenyeviti wa Serikali za Vijiji na Mitaa kutoka Halmashauri ya Msalala, Halmashauri ya Ushetu na Manispaa ya Kahama, kwa lengo la kuimarisha uwajibikaji na utoaji wa huduma kwa wananchi.


"Taifa letu, Wajibu wetu." 🇹🇿


#Kahama #FrankNkinda #SerikaliZaMitaa #Msalala #Ushetu #ManispaaYaKahama #Uwajibikaji #MigogoroYaArdhi #HudumaKwaWananchi #TaifaLetuWajibuWetu #KaziNaUtutuTunasongaMbele
Tags HABARI#

Post a Comment

0 Comments