Na Neema Nkumbi Kahama
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga (RPC), Janeth Magomi, amekutana na wananchi wa Mtaa wa Mbulu, Kata ya Mhongolo, Manispaa ya Kahama, ambapo ametoa elimu kuhusu usalama, ulinzi wa jamii na namna ya kushughulikia matukio ya ukatili wa kijinsia huku akisisitiza ushirikiano kati ya wananchi na Jeshi la Polisi katika kutokomeza uhalifu.
Akizungumza katika mkutano huo, RPC Magomi amesema Jeshi la Polisi limeelekezwa kuimarisha falsafa ya Polisi Jamii kwa kushuka moja kwa moja kwa wananchi ili kusikiliza changamoto zao na kujenga uhusiano wa karibu unaorahisisha upatikanaji wa taarifa za uhalifu.
Amesema wahalifu wanatoka ndani ya jamii, hivyo ushiriki wa wananchi katika kutoa taarifa ni silaha muhimu ya kuzuia na kupambana na vitendo vya uhalifu.
"Kazi yetu ni kulinda usalama wa raia na mali zao, Ili tufanikiwe, lazima tushirikiane na wananchi, Hatutaki tena dhana ya zamani ya kumtishia mtoto kwa kusema 'nitakuitia polisi', Tunataka wananchi watuone kama washirika wao," amesema RPC Magomi.
Katika mkutano huo, mwananchi Mary Adua Dinambo amehoji kuhusu hatua zinazopaswa kuchukuliwa na mwanamke anayenyanyaswa na mume wake nyumbani na kama kujitetea kwa kumpiga mume anayemnyanyasa ni kosa.
Akijibu swali hilo, RPC Magomi amesema ukatili wa majumbani ni kosa linaloshughulikiwa na sheria na kuwashauri waathirika kufika katika Madawati ya Jinsia na Watoto yaliyopo katika vituo vya polisi ili kupata msaada wa kisheria.
Amefafanua kuwa kumpiga mtu ni kosa la jinai, hivyo badala ya kujichukulia sheria mkononi, waathirika wanapaswa kuripoti matukio hayo kwa vyombo vya dola.
Aidha, Makoye Angelo Daudi, Mkurugenzi ameliomba Jeshi la Polisi kuendelea kutumia mikutano ya wananchi na taasisi za elimu kutoa elimu ya maadili kwa watoto na vijana ili kuzuia vitendo vya ukatili na ushawishi unaoweza kuwaingiza kwenye mazingira hatarishi.
Kwa upande wake, RPC Magomi amepokea ushauri huo na kuahidi kuwa Jeshi la Polisi litaendelea kushirikiana na shule, wazazi na viongozi wa jamii katika kutoa elimu ya kinga dhidi ya ukatili, matumizi ya dawa za kulevya na vitendo vingine vinavyohatarisha usalama wa watoto.
Pia ametumia mkutano huo kutoa elimu kuhusu haki za wananchi wanapokuwa kwenye mchakato wa kisheria, akieleza kuwa kufunga jalada la kesi kwa makubaliano ya wahusika hakutozwi fedha, na kwamba kwa mujibu wa sheria mtuhumiwa anapaswa kufikishwa mahakamani ndani ya saa 24 isipokuwa kwa makosa yanayoruhusu kushikiliwa kwa mujibu wa sheria.
RPC Magomi amesisitiza kuwa usalama wa Mkoa wa Shinyanga utaendelea kuimarika ikiwa wananchi wataendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za uhalifu na kushiriki katika juhudi za kulinda amani.
#Kahama #Shinyanga #RPCJanethMagomi #PolisiJamii #UkatiliWaKijinsia #Usalama #Mhongolo #Mbulu
0 Comments