Mbunge wa Jimbo la Itwangi, Azza Hillal Hamad, akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Mwamanyuda, Kata ya Imesela, Agosti 7, 2026, ambapo ameeleza kuwa kaya 252 za Vitongoji vya Kihongwe na Mizanza zinatarajiwa kupatiwa huduma ya umeme kupitia mpango wa kusambaza umeme ngazi ya vitongoji. Picha na Kadama Malunde
Mbunge wa Jimbo la Itwangi, Azza Hillal Hamad, akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Mwamanyuda, Kata ya Imesela, Agosti 7, 2026.
Na Marco Maduhu, SHINYANGA
Mbunge wa Jimbo la Itwangi Azza Hillal Hamad, amesema kupitia Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2025–2030, vitongoji viwili vya Kihongwe na Mizanza vilivyopo katika Kijiji cha Mwamanyuda Kata ya Imesela wilayani Shinyanga, vitanufaika na mpango wa kusambaza umeme ngazi ya vitongoji.
Amebainisha hayo leo Agosti 7, 2026, wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara wa kusikiliza kero zao na kuzitafutia ufumbuzi.
Amesema, katika vitongoji hivyo viwili, Kitongoji cha Kihongwe chenye kaya 157 na Kitongoji cha Mizanza chenye kaya 95, jumla zinakuwa kaya 252 zitakazonufaika na huduma hiyo ya umeme katika kijiji cha Mwamanyuda.
“Watu wa REA wameshafika na kufanya tathmini yao, na kinachosubiriwa ni nguzo kupelekwa na kuanza kuwekewa umeme,” amesema Azza.
Aidha, amewataka wananchi kuanza kufanya “wiring” katika nyumba zao, na kuwa tayari kulipa Sh. 27,000 kwa ajili ya kuunganishiwa huduma hiyo kwenye kaya zao.
“Nawaomba wenyeviti wa vitongoji, kuna maeneo nimekutana na changamoto kwamba wenyeviti wa vitongoji, mkikutana na watu wa REA, kuna maeneo mnaacha kuwapitisha kwenye nyumba, na nguzo zinakwenda kupita mbungani kwa ajili ya kufuata watu wawili au watatu na kuwaacha watu wengi “center”. naomba sana msifanye makosa hayo,” amesema Azza.
Aidha, amesema ndani ya miezi hiyo sita pia barabara ya Maskati–Ng’homango imeshachongwa imechongwa, ambapo awali miundombinu yake ilikuwa mibovu, hasa wakati wa masika.
Katika mkutano huo, wananchi waliuliza maswali kuhusu kukamilika kwa jengo la zahanati, ukosefu wa umeme, uchakavu wa miundombinu ya shule ya msingi Kihongwe pamoja na ukosefu wa maji safi na salama.















































0 Comments