TANGAZO

TANGAZO

WAFANYAKAZI FCC WASHIRIKI MAADHIMISHO YA MEI MOSI JIJINI DAR ES SALAAM

 

Wafanyakazi wa Tume ya Ushindani (FCC) wameshiriki kikamilifu katika Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) yaliyofanyika Leo tarehe 1 Mei, 2026 katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.

Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na mgeni rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, ambapo yamewakutanisha wafanyakazi kutoka sekta mbalimbali nchini kwa lengo la kuenzi mchango wao katika maendeleo ya taifa pamoja na kujadili ustawi wao na kuboresha mazingira ya kazi.

Wafanyakazi wa FCC wameshiriki katika maandamano sambamba na taasisi nyingine za umma na binafsi, wakionesha mshikamano wao katika kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kusimamia Ushindani wa haki unaovutia uwekezaji, ubunifu na ustawi wa soko.

Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu isemayo, “Kazi zenye staha ni nguzo imara kwa maendeleo endelevu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050,” imelenga kuhamasisha ajira zenye heshima, kulinda haki za wafanyakazi na kuimarisha mchango wao katika kufanikisha malengo ya maendeleo ya muda mrefu ya nchi.

Aidha, Maadhimisho hayo kitaifa yalifanyika Mkoani, Njombe ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Maadhimisho ya Mei Mosi hufanyika kila mwaka duniani kote kama jukwaa la kutambua mchango wa wafanyakazi katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii pamoja na kuhimiza mazingira bora na salama ya kazi.

Post a Comment

0 Comments