TANGAZO

TANGAZO

MAHAKAMA YA WILAYA YA KAHAMA YATOA FURSA KWA WAJASIRIAMALI WADOGO KUJITANGAZA WAKATI WA MAADHIMISHO YA WIKI YA SHERIA TANZANIA



Wiki ya sheria Tanzania inatarajiwa kufunguliwa rasmi January 25 mpaka Februari 3 mwaka huu 2025, ambapo mahakama ya wilaya ya Kahama katika maadhimisho hayo, imesema imedhamiria kuwainua wajasiriamali wadogo wadogo wasiokuwa na uwezo wa kujitangaza wilayani humo.


Hakimu mkazi mfawidhi mwandamizi wa mahakama hiyo Edmund Kente, akizungumza katika kikao cha pamoja na wadau wa mahakama kilichofanyika ofisini kwake Januari 10, 2025 amesema, wamedhamiria kuwainua wajasiriamali hao kwani ndio wadau wakuu wa mahakama.

“Nilivyosema kwamba mahakama na wadau, nikasema wadau wetu namba moja sisi ni wananchi, wananchi wapo kwenye shughuli zao za kujipatia kipato kila leo, kila leo, lakini pia wangependa wafahamike kwa upana zaidi, sasa je ana platform hiyo? Huenda hana” Alisema Kente

“Sasa tukasema kupitia maadhimisho ya siku ya sheria Tanzania, tuwakaribishe na hao wajasiriamali wadogo, waje na walichonacho, wanachotaka kutuonyesha sisi lakini na watu wengine kwa sababu nyinyi waandishi wa Habari mtakuwepo, mtawatangaza, kuliko kumfuata mtu mmoja mmoja anaishi sijui Igomelo, akiwa hapa mahakamani anakuwa na nafasi kubwa zaidi ya kuonekana kuliko akiwa huko mtaani kwake” Aliongeza Kente

Wakati huo huo Kente amewatahadharisha vishoka (Bush-Lawyers) na kwamba ni wahalifu kama wahalifu wengine, hivyo mahakama hiyo haiku tayari kuona wahalifu wa namna hiyo wakiendelea kuwaibia wananchi.

“Lakini nashukuru kupitia wiki ya sheria mwaka jana, tuliweza ku-addres hii ishu mpaka wakati huu unavyouliza swali hili sijawasikia tena, tuliweza kuweka mikakati kwamba wananchi kwanza watoe taarifa, lakini mtu ikitokea akikamatwa tuweze kumshughulikia kikamilifu” Alisema Kente 

Nao baadhi ya wadau wa mahakama waliohudhuria kikao hicho akiwemo Jeremiah Madama Territory meneja kutoka Yas (Tigo), na Bhoke Matiko afisa mahusiano wa Azania Bank tawi la Kahama, wameishukuru mahakama hiyo kwa hatua ya kuwashirikisha wadau katika wiki hii ya sheria kwani itawarahisishia wao kuwafikia wateja wao kwa wakati na urahisi zaidi kama wakiwa ofisini.

“Tunashukuru sana kwa kupata nafasi hii kubwa sana ya kushiriki maana kwanza kabisa elimu ambayo sisi tunatamani kuifikisha kwa wananchi, ambayo pia imekuwa ikihusisha sana mahakama, watu wengi wamekuwa wakifikishwa mahakamani, kwa sababu ya makosa ya kimtandao” Alisema Jeremiah

“Labda mtu amepata line ambayo haikuwa na majina yake halafu mwisho wa siku kukawa kuna kosa limefanyika, lakini pia si hapo tu kuna baadhi ya watu pia wanaachia NIDA zao zinatumika vibaya, watu wanasajiliwa lakini yule anayekwenda kutumia ile anakwenda kufanya uhalifu, kwa hiyo unaweza kukuta ni mzee anatafutwa, anakamatwa, lakini ukiangalia unagundua kwamba hakua anahusika kwa namna yoyote ile” Aliongeza

“Kwa hiyo sisi kama wadau wa ubia na mahakama wa kimawasiliano tuko tayari kabisa tumejiandaa kwa ajili ya hiyo wiki kuanzia tarehe 25 mpaka tarehe 3, kutoa elimu iweze kuwafikia wananchi, na tunaamini kama mahakama ambavyo imekuwa na lengo la kuhakikisha kwamba inaanza mwaka vizuri na wananchi kupata elimu, basi tunaamini elimu hii itafika vizuri sana, tutajitahidi tutatuma broadcast sms kwa wananchi, lakini pia tutajitahidi hapa na pale watu watakapokuwa wanatutembelea katika banda letu, tutatoa elimu sambamba na ile elimu ambayo mahakama inakusudia kutoa” Alisema Jeremiah

“Utaratibu wa mahakama kuwashirikisha wadau, kuelekea wiki hii ya sheria ambayo itaanza tarehe 25 mwezi huu wa kwanza 2025, sisi kama benki tumeipokea vzr, ni utaratibu mzuri sana, na sisi kama Azania bank ambao ni wadau mahsusi kabisa, tumeipokea vizuri na tunaahidi kushirikiana pamoja na mahakama kwa sababu tunapata manufaa mengi sana” Alisema  Bhoke

“Kupitia wiki hii ya sheria, sisi kama benki tunaweka tent letu pale, tutapata wateja, wa kufungua account, lakini pia tunatoa elimu kwa wateja ambao wanafika katika maadhimisho haya kuhusiana na mambo ya kibenk lakini pia mikopo, kama wadau tunaipokea vizuri sana huu ni utaratibu mzuri” Aliongeza Bhoke

“Wito wangu kwa wadau wote ni kwamba waweze kufika wakashiriki katika wiki hii, wiki hii ina manufaa makubwa haswa kwa sisi wadau, kila mdau kwa nafasi yake aweze kushiriki afike kuna manufaa mengi ambayo atayaoata hapa” Alisema Bhoke

Kauli mbiu ya wiki ya sheria mwaka huu 2025 inasema,, Tanzania ya 2050, nafasi ya taasisi zinazosimamia haki-madai katika kufikia malengo makuu ya dira ya Taifa ya maendeleo

Katika uzinduzi wa wiki ya sheria, mahakama ya wilaya ya Kahama itaanza na matembezi ya amani kuanzia viwanja vya mahakama ya mwanzo na kutamatika katika viwanja vya mahaka ya wilaya Januari 25, 2025, yakiongozwa na mkuu wa wilaya ya Kahama Mboni Mhita, na kuwashirikisha wananchi wote, lakini pia ni sehemu ya mazoezi ili kuepuka magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

Hakimu mkazi mfawidhi mwandamizi wa mahakama ya Wilaya ya Kahama Edmund Kente. 

Post a Comment

0 Comments