TANGAZO

TANGAZO

FAMILIA YA MZEE LUKUBA YA NGULU KAHAMA, YANUAFAIKA NA MIKOPO YA 10% YA MAKUSANYO YA NDANI YA HALMASHAURI



Bi. Sophia Emanuel akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake kuhusu mikopo ya asilimia kumi ya  halmashauri na vile alivyoweza kunufaika nayo.


KAHAMA

Familia ya Mzee Lukuba Washa ya kijiji cha Ngulu Kata ya Ngogwa Manispaa ya Kahama ni miongoni mwa familia zilizonufaika na mikopo ya asilimia kumi ya makusanyo ya ndani ya Halmashauri ya manispa ya Kahama mkoani Shinyanga, ambapo kupitia mikopo hiyo, familia hii inafanikiwa kujenga nyumba ya kisasa na kununua ng'ombe watano, sambamba na kufanya kilimo cha kisasa kinachoiwezesha familia hii kutoka katika wimbi la umasikini.

Hii ni baada ya Bi Sophia Emanuel ambaye ni mke wa mzee Lukuba, kujiunga na kikundi cha wanawake cha hisa, na baadae kupata taarifa na elimu na mikopo hii kutoka kwa afisa maendeleo ya jamii wa kata ya Ngogwa Esther Sanga, na baadae kuipata fursa hii iliyoinufaisha familia yake.


Akizungumza nyumbani kwake wakati wa ziara ya waandishi wa habari, Bi Sophia, amesema kuwa walianza kwa kuunda kikundi cha wanawake cha kuweka hisa, ambapo walipokuwa wakifanya shughuli za kijamii, walijua kuhusu mikopo ya halmashauri kutoka kwa afisa maendeleo.


"Tulikuwa na kikundi cha wanawake tukiweka hisa, ndipo tuliposikia kwamba halmashauri inatoa mikopo, tukaenda kwa afisa maendeleo na akatuelekeza. Baada ya kupata maelekezo, tukaamua kuanza kukopa mikopo hiyo," alisema Sophia.


Sophia ameongeza kuwa mikopo hiyo imewasaidia sana, hasa kwa kuwa wanafanya shughuli za kilimo kama vile kulima vitunguu, pamoja na kununua mbunga kwa bei nafuu na kuuza kwa bei kubwa, jambo ambalo limewawezesha kurudisha mikopo hiyo bila usumbufu.


"Kwa kweli, mikopo hii imetusaidia sana. Familia yangu sasa ina nyumba ya kisasa na pia nimenunua ng'ombe watano ambao wanatusaidia kulima na kupata maziwa," alisema Sophia.


Baba wa familia hiyo, Mzee Lukuba, amekiri kuwa awali alipokuwa akisikia kuhusu mikopo ya halmashauri, alijawa na wasiwasi, lakini alikubali mkewe kushiriki kwa sababu aliona faida kwa familia yao, Mzee Lukuba amewashauri wanaume wenzake kuwaachia wake zao kushiriki katika vikundi vya kifedha ili nao wanufaike, kwani vikundi vya aina hii vinasaidia sana.


Kwa upande mwingine, Samwel Samson, kijana kutoka katika jamii hiyo, amesema kuwa wao kama vijana wamehamasishana kuchangamkia fursa za mikopo, na kwamba vikundi vikiwa na vigezo vinavyotakiwa, wanapaswa kupatiwa mikopo bila ubaguzi.


Afisa maendeleo ya jamii wa kata ya Ngogwa, Esther Sanga, ambaye ni mshauri wa vikundi vya kifedha katika eneo hilo, amesisitiza kuwa kazi yake kubwa ni kuhamasisha jamii kuondokana na mawazo hasi na kujiunga na vikundi ili waweze kupata mikopo ya asilimia kumi ya halmashauri.


"Awali, wanawake walikuwa wanajiunga na vikundi na kukopa bila kushirikisha waume zao, hali ambayo ilileta migogoro familia kwa familia," amesema Ester. "Hata hivyo, nimeendelea kuwaelimisha, na sasa nawashauri wanawake kushirikisha waume zao ili kuepuka matatizo, Sasa hatutatoa tena mikopo kwa mwanamke ambaye hatamshirikisha mume wake au familia kwa ujumla."


Ester ameongezea kuwa mikopo hii siyo kwa wanawake pekee, bali pia kwa vijana na walemavu, na kwamba wanapaswa kujiunga ili waweze kunufaika na mikopo hiyo.


Mikopo hii ya asilimia kumi ya halmashauri imekuwa na manufaa makubwa kwa familia nyingi, na imechangia kuboresha maisha ya wananchi kwa kuwapa fursa ya kujenga, kuwekeza katika kilimo, na biashara.


Kwa mwaka wa fedha 2024/2025 Halmashauri ya Manispaa ya Kahama imetenga zaidi ya shilingi milion 870 kwa ajili ya vikundi vya ujasiriamali vya wanawake, vijana na wenye ulemavu ambayo ni asilimia kumi ya makusanyo ya ndani ya Halmashauri hiyo.

Bi Sophia akiwa amesimama katika nyumba yake huku akifurahia mafanikio yake
Nyumba kubwa na imara, iliyo na paa la kisasa la mabati, madirisha ya vioo na milango ya kisasa, ikionesha ubora wa ujenzi.
Nyumba kubwa na imara, iliyo na paa la kisasa la mabati, madirisha ya vioo na milango ya kisasa, ikionesha ubora wa ujenzi.
Nyumba aliyokuwa akiishi Mzee Lukuba na Familia yake kabla ya kujenga nyumba ya kisasa
Afisa maendeleo kata ya Ngogwa akielezea jinsi anavyotoa elimu katika vikundi vilivyopo katika kata yake 
Mzee Lukuba akizungumza na waandishi wa habari juu ya mafanikio waliyoyapata kupitia mikopo ya asilimia 10
Mzee Lukuba akiwa na mke wake wakiwa wamekaa, Wanaonekana wakiwa na nyuso za furaha huku wakifurahia mafanikio waliyoyapata

MWISHO.

Post a Comment

0 Comments