TANGAZO

TANGAZO

WADAU WALIA NA MICHEZO YA ASILI KAMA ‘BABA NA MAMA’

 


Wanafunzi wa TASUBA wakiwakaribisha wageni kwa ngoma kabla ya mdahalo.
Mzee wa Mila wilayani Bwana Mwinyi Hashimu Akida akizungumza
Wadau wakisaini ahadi ya kukuza Urithi wa Utamaduni Usioshikika mjini Bagamoyo 
Wadau wakifurahia ngoma

Na Mwandishi wetu, Bagamoyo

Wadau wanaofanya kazi za kudumisha Utamaduni wa Urithi Usioshikika wamesisitiza jamii kuendelea kuenzi michezo ya asili ili kutengeneza jamii ya watu wanaowajibika.

Michezo hiyo ukiwemo ule wa Baba na Mama inaaminika kuwa ilisaidia makuzi ya mtu kujua majukumu yake kama mwanaume na mwanamke.

Ushauri huo ulitolewa mjini Bagamoyo wakati wa mdahalo wa vijana uliolenga kuwajengea uwezo wa namna ya kukuza Urithi wa Utamaduni Usioshikika katika nyakati hizi za kidijitali

Akichangia mjadala huu, bwana Anthony Tiluganilwa mdau kutoka TASUBA alisema michezo ya asili ilikuwa inawafundisha kujitegemea kwani walicheza nje bila wazazi na hivyo kudumisha upendo na watoto wengine tofauti na sasa ambapo watoto wengi wanafungiwa magetini.

“ Tulipocheza kama Baba na Mama, mwanamke aliigiza majukumu ya mama na wa kiume aliigiza majukumu ya Baba. Jambo hili lilisaidia sana kwani hadi tumekua tunajua majukumu yetu. Kwa sasa hili halifanyiki matokeo yake tuna watu wabinafsi na wanaokwepa majukumu yao,” alisema Tiluganilwa.

Akichangia mjadala huo, mzee wa mila na mwenye ushawishi wilayani Bagamoyo bwana Hashimu Ally Kida alisisitiza umuhimu wa kukifundisha kizazi cha vijana ili kujua tulikotoka.

“Ni vema tukaongeza juhudi za kujadiliana ili kizazi chetu kijue mila zetu na desturi ili kujua tulikotoka katika tamaduni zetu,” alisisitiza Mzee Akida.

Kwa upande wake Angela Kidwanga, mwanafunzi wa TASUBA alisisitiza umuhimu wa wazazi kuwafundisha Watoto kujitegemea ili kukwepa vijana kupenda mashangazi ( Wanawake waliowazidi umri) na mabinti kutafuta sponsors ( wanaume watu wazima) badala ya kufanya kazi.

“ Naomba niwashauri wazazi pia wawe wanawapeleka Watoto kijijini walikotoka ili wajue mila na utamaduni wao kuliko kuwaacha mijini. Vilevile tunaomba watufundishe lugha zetu za asili badala ya kutumia Kiingereza tu,” alisema Kidwanga.

Urithi wa Utamaduni Usioshikika unajumuisha ujuzi na maarifa ya kiutamaduni katika jamii ikiwemo ujuzi wa kucheza ngoma za asili, kuandaa vyakula vya asili na namna ya kujieleza ikiwemo lugha ambapo inasemekana lugha nyingi za asili zipo hatarini kupotea kutokana na wazazi kushindwa kurithisha kwa watoto wao.

Majadiliano haya yaliandaliwa na UNESCO kwa kushirikiana na serikali ili kuchagiza urithishwaji wa utamaduni usioshikika na namna ambavyo unaweza kuchagiza ajira na kuongeza kipato hususani katika nyakati hizi za kidijitali.

Post a Comment

0 Comments