Mkuu wa wilaya ya Kahama, Mhe. Mboni Mhita akiongea na wadau mbalimbali baada ya kumaliza ziara ya kutembelea mgodi wa Barrick Buzwagi uliofungwa.
Mkuu wa wilaya ya kahama Mhe. Mboni Mhita, akibadilishana mawazo na Balozi wa Utalii wa Ndani, Emmanuel Mgaya, wakati wa ziara ya kutembelea Buzwagi.
Mkuu wa wilaya ya Kahama Mhe. Mboni Mhita, akibadilishana mawazo na Balozi wa Utalii wa Ndani, Emmanuel Mgaya, wakati wa ziara ya kutembelea Buzwagi.
***
Serikali wilayani Kahama mkoani Shinyanga, imepongeza kampuni ya Barrick nchini kwa kuendesha ufungaji wa mgodi wa Barrick Buzwagi kwa viwango vya kimataifa kiasi kwamba eneo limewekwa katika mazingira bora na linaonyesha mwelekeo wa kuwa kitovu cha kukuza uchumi mkoani Shinyanga na nchi jirani.
Akiongea wakati wa ziara ya kutembelea eneo hilo lililokuwa mgodi wa Buzwagi, Mkuu wa wilaya ya Kahama,Mhe. Mboni Mhita, ambaye aliongozana na viongozi mbalimbali wa Serikali alisema uendelezaji wa kulifanya eneo hilo kuwa eneo maalumu la uwekezaji ambalo litajulikana kama ukanda maalum wa kiuchumi wa Buzwagi (Buzwagi Special Economic Zone) ni wa kuridhisha na amewataka wawekezaji kuchangamkia fursa kwa kuwekeza katika eneo hilo.
"Barrick imeendesha zoezi la kufunga mgodi huu kwa weledi mkubwa na kuiweka sehemu hii katika mazingira bora na endelevu ambayo yataendelea kuleta manufaa kwa jamii inayozunguka eneo hili la Buzwagi. Serikali iko tayari kuwapa ushirikiano wakati wote wawekezaji wanaotaka kuwekeza katika Buzwagi Special Economic Zone, ambayo tayari imeishaanza kuwa na mwekeleo kwa kuwa kitovu cha biashara katika mikoa ya kanda ya ziwa na nchi jirani na kuchochea ukuaji wa uchumi", amesema.
Mhe. Mboni amesema Serikali inajivunia ushirikiano uliopo baina ya yake na Kampuni ya Barrick, Kwani tayari baadhi ya Wawekezaji wameanza kuwekeza katika Mradi huo na kuzalisha fursa za ajira kwa Watanzania sambamba na kuchangia pato la Serikali kupitia ilipaji wa kodi mbalimbali.
Kwa upande wake Meneja wa Ufungaji Mgodi wa Barrick Buzwagi, Zonnastral Mumbi, amesema Barrick itaendelea kushirikiana na Serikali wakati wote kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa viwango vya kimataifa na kuwa mfano wa kuigwa kwa kufunga shughuli za mgodi na kuacha eneo lililokuwa mgodi linakuwa na miradi endelevu ya kuwanufaisha Wananchi na taifa kwa ujumla.
“Jukumu la Kampuni endelevu ya uchimbaji madini si kutengeneza thamani kwa wadau wakati uliopo bali pia ni kuhakikisha kuwa inaacha urithi mzuri ambao utaendelea kuhudumia jamii kwa muda mrefu baada ya uchimbaji kufikia mwisho katika mgodi wa Barrick Buzwagi”,amesema Mumbi.
Naye Balozi wa Utalii wa Ndani, Emanuel Mgaya,ambaye alikuwa kwenye ujumbe wa Serikali uliotembelea eneo hilo,alisema ufungaji wa mgodi huo umefanyika kwa weredi mkubwa na Barrick imeacha alama ya kudumu ambayo itakumbukwa mpaka vizazi vijavyo na aliwataka Wawekezaji wa Tanzania kutobaki kunywa katika uwekezaji katika eneo hilo badala ya kubaki nyuma na kudhani limetengwa kwa ajili ya wawekezaji wa nje pekee.
Katika kuboresha zaidi eneo hilo kibiashara kampuni ya Barrick imejenga jengo jipya la abiria katika uwanja wa ndege Uwanja wa Ndege wa Mgodi uliofungwa wa Buzwagi lenye uwezo wa kuhudumia zaidi ya abiria 200 kwa wakati mmoja ikilinganishwa na abiria 25 tu hapo awali na tayari limekabidhiwa kwa Serikali.
Mgodi wa dhahabu wa Buzwagi ulikuwa kitovu cha uchumi wa mkoa wa Shinyanga nchini Tanzania kwa takribani miaka 15 ambapo katika kilele chake, Buzwagi ulikuwa mgodi wa pili kwa ukubwa nchini Tanzania na uliajiri watu 3,000 na maisha yake ya uendeshaji yalifika tamati Julai 2021 na mgodi huo ulifungwa rasmi Julai 2022.
0 Comments