TANGAZO

TANGAZO

TAKUKURU YASIKITISHWA NA UPUNGUFU WA TAARIFA ZA RUSHWA YA NGONO


Mkuu wa Dawati la Uzuiaji Rushwa kutoka TAKUKURU Mkoa wa Manyara, Paschal Mhagama

Licha ya kuendelea kuwepo kwa vitendo vya rushwa ya ngono katika jamii, muamko wa waathirika kutoa taarifa kwa vyombo husika umekuwa mdogo, na wengi wao wamekuwa wakiishi na mateso kwa kutotoa ushirikiano kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

Hayo yamesemwa leo Jumatatu Novemba 25 na Mkuu wa Dawati la Uzuiaji Rushwa kutoka TAKUKURU Mkoa wa Manyara, Paschal Mhagama, wakati akiwasilisha mada kuhusu rushwa ya ngono na madhara yake katika uzinduzi wa kampeni maalum ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia iliyofanyika mkoani Manyara.

Mhagama amefafanua kuwa, mwaka 2023, makosa ya rushwa ya ngono yaliyoripotiwa kwa TAKUKURU yalikuwa 28 pekee kwa nchi nzima, licha ya kuwepo kwa vitendo hivyo katika jamii.

 Ameeleza kuwa hali hii inatokana na uoga na aibu kutoka kwa waathirika wa matukio ya ukatili, ambao mara nyingi hushindwa kutoa taarifa kwa mamlaka.

"Jamii inapaswa kutoa ushirikiano kwa TAKUKURU kwa kutoa taarifa pale wanaposhuhudia au kukutana na vitendo vya rushwa ya ngono. Ushirikiano wa wananchi ni muhimu katika kupambana na hali hii ya kikatili," amesema Mhagama.

Mkuu huyo wa dawati ameongeza kuwa, bila ushirikiano wa jamii, vita dhidi ya rushwa ya ngono haitafanikiwa, na kwamba kila mwanajamii ana jukumu la kuzuia na kukomesha vitendo hivi vinavyohatarisha haki za binadamu.


TAKUKURU imeendelea kuhamasisha jamii kuchukua hatua za kutoa taarifa kwa wakati, huku ikisisitiza umuhimu wa kudhibiti vitendo vya rushwa ya ngono ambayo hufanyika katika maeneo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kazini, shule, na jamii kwa ujumla.

Maadhimisho haya yameratibiwa na Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) kwa kushirikiana na Klabu ya Waandishi wa Habari wa Mkoa wa Manyara.

Post a Comment

0 Comments