TANGAZO

TANGAZO

Video...DIWANI KAHAMA MJINI ATEMBELEA MASOKO, VIJIWE VYA BODABODA NA VITUO VYA MABASI KUHAMASISHA USAFI KUKABILI ATHARI ZA EL NIÑO

 


Diwani wa Kahama Mjini Godson Andrew akizungumza na wafanyabiashara wa mbogamboga katika soko la Namanga, Manispaa ya Kahama, akihamasisha usafi wa mazingira na utunzaji wa mitaro ya maji kuepuka magonjwa na athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Nino.




Diwani wa Kahama Mjini Godson Andrew akizungumza na maafisa usafirishaji (bodaboda), Manispaa ya Kahama, akihamasisha usafi wa mazingira na utunzaji wa mitaro ya maji kuepuka magonjwa na athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Nino.


🌟KAHAMA.


Diwani wa Kata ya Kahama Mjini, Goldson Andrew, amewataka wananchi, wafanyabiashara na wajasiriamali kuimarisha usafi wa mazingira, ikiwemo kusafisha mitaro na kuondoa taka ngumu, ili kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua kubwa zinazotarajiwa kuelekea mwisho wa mwaka.

 

Ametoa wito huo alipotembelea na kuhamasisha usafi wa mazingira katika soko kuu la wakulima la Namanga Manispaa ya Kahama.

 

Amesema taarifa za wataalamu zinaonesha uwezekano wa mvua kuwa juu ya wastani, hivyo wananchi wanapaswa kuchukua hatua mapema kuhakikisha maeneo wanayoishi, wanayofanyia biashara, mitaro na mifereji ya maji inakuwa safi na wazi.

 

Amesema usafi ni muhimu husuani katika maeneo ya masoko na vituo vya mabasi ambavyo vina mitaro inayohitaji kutunzwa mara kwa mara ili kuzuia taka kuingia na kuziba njia za maji, jambo linaloweza kuongeza hatari ya maji kutuama au kusababisha mafuriko wakati wa mvua hizo.

 

“Ni lazima mitaro yetu yote ifunguke na pia tuhakikishe mitaro hii inakuwa misafi. Jiografia ya masoko yetu na stendi ina mitaro, hivyo ni muhimu kuhakikisha taka hazizuii upitishaji wa maji,” amesema Endru.

Amesema licha ya kuwa kata hiyo imeweka utaratibu wa kufanya usafi kila Jumamosi kuanzia saa 12 asubuhi hadi saa tatu asubuhi, bado wananchi wanalo jukumu la kuhakikisha maeneo yao yanakuwa safi wakati wote.

 

Andrew amesema moja ya changamoto inayohitaji kushughulikiwa ni baadhi ya wafanyabiashara wa maduka na fremu kuchelewa kufungua biashara siku za Jumamosi ya usafi bila kufanya usafi, hali inayowafanya kukosa muda wa kushiriki katika zoezi hilo.

 

Amesema wafanyabiashara wanapaswa kuwahi asubuhi, kufungua biashara zao baada ya kufanya usafi wa maeneo yao, ikiwemo mitaro, sehemu za mbele ya maduka na maeneo ya kazi, badala ya kutegemea wafanyakazi wa usafi wa Manispaa.

 

Diwani Andrew amewapongeza wananchi wa Kata hiyo, hususan wafanyabiashara wa Soko la Namanga na Stendi Kuu, kwa kuunga mkono jitihada za Rais Dkt Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha mazingira yanakuwa safi wakati wote.

 

Amesema uongozi wa kata pia unashirikiana na mzabuni wa ukusanyaji taka ili kuongeza mzunguko wa zoezi la kuzoa taka ngumu kutoka mara moja kwa wiki hadi kila baada ya siku mbili au tatu, kwa lengo la kuzuia mrundikano wa taka unaoweza kusababisha mitaro kuziba.

 

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Soko la Namanga, Yahaya Juma, amesema usafi sokoni hapo unaridhisha kutokana na ushirikiano wa viongozi wa Serikali na wafanyabiashara.

 

Juma amesema ushiriki wa viongozi na wananchi umewezesha usafi kuimarika, huku akieleza kuwa juhudi za kuhakikisha soko linaendelea kuwa safi zinapaswa kuendelea hata baada ya siku maalumu ya usafi.

 

Naye mfanyabiashara katika Soko la Namanga, Christina Mpelwa, amesema usafi katika eneo hilo umeanza kuleta mabadiliko, ikiwemo kuboresha mazingira na hali ya hewa kwa wafanyabiashara na wananchi wanaofika sokoni.

 

Amesema “Usafi kwetu ulikuwa kero, lakini kwa sasa tunaendelea vizuri. Nimeingia hapa nimeona mambo ni mazuri, hata hewa nimeona ni nzuri kuvuta.”



 

Post a Comment

0 Comments