TANGAZO

TANGAZO

Video: ZAIDI YA SH MILIONI 700 KUKARABATI VITUO VYA AFYA/ZAHANATI KUBORESHA HUDUMA KITUO CHA AFYA NYASUBI, KAHAMA





KAHAMA.


Serikali imetoa zaidi ya Shilingi milioni 700 kwa ajili ya kuboresha na kukarabati vituo vya afya na zahanati, ili kupunguza msongamano wa wagonjwa katika Hospitali ya Manispaa ya Kahama pamoja na Kituo cha Afya Nyasubi mkoani Shinyanga.


Mbunge wa Kahama Mjini, Benjamin Ngayiwa, amesema hayo katika mkutano wa hadhara uliofanyika Mtaa wa Mbulu, kata ya Mhongolo, wakati yeye na Diwani wa Kata hiyo, Mariam Ngalula, walipofika kusikiliza na kutatua kero za wananchi waliowaamini na kuwachagua katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.




Ngayiwa amesema serikali tayari imepeleka Sh milioni 200 kwa ajili ya kuboresha Kituo cha Afya cha Isagehe, Sh milioni 200 kituo cha Afya cha Nyandekwa na Sh milioni 200 kituo kingine cha afya, na kwamba hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za kusogeza huduma za afya karibu na wananchi.



Amesema sambamba na ukarabati wa vituo hivyo, Serikali inaendelea na maboresho ya Zahanati ya Mhungula, ambayo ipo katika hatua za awali za ujenzi, huku mipango ikiendelea kwa ajili ya kukamilisha jengo hilo na kulipatia vifaa tiba ili lianze kutoa huduma.



Amesema maboresho hayo yanalenga kuhakikisha wananchi wanapata huduma karibu na maeneo yao, badala ya kulazimika kwenda Hospitali ya Manispaa ya Kahama kwa huduma ambazo zinaweza kutolewa katika vituo vya afya vilivyo karibu nao.

Amesema “Tunataka tuboreshe vituo vya afya vilivyopo pamoja na kuongeza vituo vingine vya afya ili kupunguza msongamano katika hospitali yetu ya manispaa na kituo cha afya Nyasubi ambacho kinaonekana kuzidiwa. Rais Samia ametoa fedha za kutosha.”



“Tumegundua huduma katika hospitali yetu ya Manispaa ya Kahama haziridhishi, tumeshaongea na mganga mkuu, mfawidhi pamoja na mkunga mfawidhi na tumekubaliana kupunguza kiwango cha malalamiko ya wagonjwa.” Ameongeza


Ngayiwa amesema wamekubaliana na wataalamu wa afya kuongeza ubora wa huduma kwa kupunguza muda wa mgonjwa kukaa hospitalini na kuboresha namna wagonjwa wanavyopokelewa na kuhudumiwa.


Awali, Diwani wa kata ya Mhongolo, Mariam Ngalula, alisema amerejea mbele ya wananchi kwa moyo wa shukrani baada ya kumchagua na kumpa nafasi ya kuwa mwakilishi wao katika uchaguzi wa Oktoba 2025.


Ngalula aliwataka wananchi kuendelea kushirikiana na viongozi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, akisisitiza kuwa ushirikiano wao ni muhimu katika kuhakikisha Kata ya Mhongolo inasonga mbele kimaendeleo.










Post a Comment

0 Comments