
Na Neema Nkumbi, USHETU
Shule ya Sekondari Ushetu, iliyopo katika Halmashauri ya Ushetu, Wilaya ya Kahama, Mkoa wa Shinyanga, imeomba msaada wa upatikanaji wa maji tiririka na kompyuta ili kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia shuleni.
Ombi hilo limetolewa kupitia risala ya wanafunzi wa kidato cha nne katika mahafali ya 15 ya shule hiyo, iliyosomwa na Roda Reuben ambapo wameeleza kuwa ukosefu wa maji ya uhakika ni miongoni mwa changamoto zinazowakabili wanafunzi.
Roda amesema kuwa baadhi ya wanafunzi hulazimika kutumia maji yasiyo salama, hali ambayo inaweza kuhatarisha afya zao na kuathiri mchakato wa kujifunza.
Aidha, wanafunzi wameomba shule hiyo ipewe kompyuta, wakieleza kuwa ukosefu wa vifaa hivyo unawapa changamoto wanafunzi wanaosoma somo la Kompyuta kwa kuwa shule haina kompyuta hata moja kwa ajili ya mafunzo ya vitendo.
Akijibu risala hiyo kwa niaba ya Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Emanuel Cherehan, Katibu wake Richard Gwesa, ameahidi kushughulikia suala la kompyuta na kuhakikisha shule inapata kompyuta kabla ya mwisho wa mwaka huu.
“Kuna upungufu wa computer kwenye shule hii, Kuna uhitaji wa computer kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo, Mwalimu Mkuu na wazazi kwa ujumla, naomba hili nichukue tutalitekeleza na tutakamilika kabla ya mwaka huu kuisha,” amesema Gwesa.
Amesema ofisi ya Mbunge itaendelea kufanya mawasiliano na uongozi wa shule ili kuhakikisha ahadi hiyo inatekelezwa kabla ya Desemba 2026.
Kwa upande wa maji, wanafunzi wameendelea kuiomba Serikali, viongozi na wadau wa maendeleo kushirikiana na shule kuhakikisha inapata maji tiririka na salama, hatua itakayosaidia kuboresha afya na mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi.
Mkuu wa shule ya sekondari U, Ellen Doto, amewataka wazazi kuacha tamaa ya kupata mali kupitia watoto wao, akisisitiza kuwa elimu ni uwekezaji muhimu kwa maisha ya mtoto.
Shule ya Sekondari Ushetu ilianzishwa mwaka 2009 na mwaka huu imefanya mahafali yake ya 15, huku wanafunzi 40 wakihitimu kidato cha nne.
USHETU SECONDARY — ONE IS HERE! 🎓











0 Comments