TANGAZO

TANGAZO

Tazama Video: DIWANI MAHONA ASIMIKA VIJANA 150 WA JESHI LA JADI (SUNGUSUNGU) , AWATAKA KUSHIRIKIANA NA VYOMBO VYA ULINZI KUDHIBITI UHALIFU

 

Diwani wa kata ya Segese Patrick Mahona akiwavisha nishani vijana waliohitimu mafunzo ya jeshi la jadi katika kijiji cha Segese namba moja kata ya Segese halmashauri ya Msalala, wilayani Kahama mkoani Shinyanga.

 

Wananchi wa kata ya Segese, Halmashauri ya Msalala, mkoani Shinyanga, wametakiwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama ili kudhibiti matukio ya uhalifu yanayochelewesha maendeleo katika maeneo yao.

 

Wito huo umetolewa na Diwani wa Kata ya Segese, Mheshimiwa Patrick Mahona, wakati wa hafla ya kuwasimika vijana wa Jeshi la Jadi la Sungusungu iliyofanyika kijiji cha Segese namba moja.

 

Akizungumza katika hafla hiyo, Diwani Mahona alisisitiza kuwa uwepo wa wahalifu ni kikwazo kikubwa kwa juhudi za maendeleo ya wananchi.

 

‘’Suala la ulinzi ni letu sote. Pale ambapo maendeleo yanakuwepo na uhalifu unaongezeka, naamini hawa vijana watatusaidia. Na sisi viongozi tunaahidi kushirikiana nanyi, tukiwa salam tutavutia wawekezaji kwa maendeleo yetu.” Amesema Mahona

 

Kwa upande wake, Mkuu wa Kituo cha Polisi Kata ya Segese, mkaguzi Nimrodi Swai, aliwaasa wahitimu hao na wanachama wengine wa Jeshi la Jadi la Sungusungu kuzingatia mafunzo waliyopewa.

 

“Niwaombe yale yote mliyofundishwa muyashike na kuyazingatia. Hayo ndio ambayo yatakuwa nguzo katika utendaji kazi wenu wa kila siku katika kazi za ulinzi na usalama.” Amesema Swai

 

Sungusungu: Nguvu ya Wananchi

 

Wananchi wa kata ya Segese wameeleza namna Jeshi la Sungusungu lilivyokuwa msaada mkubwa katika kulinda mali na usalama wao.

 

Mmoja wa wananchi hao, Abel Bondo, pamoja na mhitimu wa mafunzo hayo, Ismail Andrea, wamesema:

 

“Jeshi la Sungusungu kwa sisi wananchi lina faida kubwa sana. Wahalifu waliwahi kuvamia kwenye kibanda changu usiku lakini Sungusungu waliwahi. Nilipigiwa tu simu kwamba wameshawadhibiti.”

 

Vijana 150 Wahitimu

 

Katika mafunzo hayo, kati ya vijana 240 waliotaka kujiunga na Jeshi la Jadi la Sungusungu katika Kijiji cha Segese Namba 1, vijana 150 wamehitimu na kuahidi kushirikiana na vyombo vya ulinzi katika kulinda amani na usalama wa kijiji na kata yao kwa ujumla.

 

Hatua hiyo inatarajiwa kuimarisha ulinzi wa kijiji na kutoa mazingira rafiki kwa wawekezaji, biashara na shughuli za maendeleo.

 

























Post a Comment

0 Comments