TANGAZO

TANGAZO

TANESCO YAFANYA OPERESHENI MGODINI, YABAINI WACHIMBAJI WAKIIBA UMEME KAHAMA

 

Na Mwandishi wetu ,KAHAMA.
 
SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoani Shinyanga, mapema leo imefanya operesheni maalumu katika Mgodi wa Mwime uliopo kata ya Zongomela Manispaa ya Kahama na kuwabaini baadhi ya wachimbaji wadogo kuchepusha umeme na kuwaunganishia wengine kinyemela.
 
Operesheni hiyo imeongozwa na Ofisa Usalama wa Miundombinu wa Shirika hilo, Mhandisi Frank Njavike na kuwabaini wachimbaji 11 ambao wamechepusha umeme na kuwaunganisha wengine kinyemela, hatua ambayo inasababisha serikali kuendelea kupoteza mapato yake.
 
Akizungumza na Malunde 1 Blog katika eneo la tukio amesema, Operesheni hiyo imeanza katika mgodi wa Mwime na baadae itaelekea katika maeneo mbalimbali wilayani Kahama na inalenga kuwabaini na kuwaibua wale ambao wanajiunganishia huduma bila kufuata utaratibu uliowekwa kisheria.
 
Amesema,kitendo cha wachimbaji kuchepusha umeme usiingie kwenye mita pamoja na kuwaunganishia huduma hiyo wengine ni kosa na hakipaswi kuvumilika kwani kinasababisha serikali kuendelea kukosa mapato yake na hawa waliobainika sheria itachukua mkondo wake.


 
“Kila aliyepata huduma kinyemela atawajibika kisheria na adhabu zinatofautina. Niwatake wachimbaji wanapotaka huduma hii wafuate sheria za kupata huduma zilizowekwa nasio kuchepusha na kulishababishia hasara shirika”,amesema Mhandisi Frank.
 
Naye Mhandisi wa Mapato wa Shirika hilo, Mgeta Majula amesema wamebaini wachimbaji 11 ambao wamechepusha umeme na kuwaunganishia wengine kinyemela.
 
Amesema,waliobainika wamechepusha umeme kutoingia kwenye mita na kuutumia moja kwa moja, kugawa umeme kwa watu wengine pamoja na kujenga line mpya kutoka upande mmoja, jambo ambalo ni hatari na kunaweza kusababisha kuwaka moto.
 
Aidha amewataka wachimbaji kutumia umeme katika matumizi sahihi, wasiwe wezi na kuwaunganishia huduma hiyo watu wengine kwani wanapobainika wanachukuliwa hatua za kisheria zinazosababisha kupunguza mitaji yao au kwenda jela na kushindwa kuzalisha mali.
 
Ofisa Mahusiano na Huduma kwa wateja wa Shirika hilo, Emma Nyaki  amesema, baadhi ya wateja wamekuwa hawafuati taratibu za kupata huduma ya umeme na badala yake wanajiunganishia kinyemela au kuunganishiwa na watu wengine 'vishoka' jambo ambalo sio sahihi.
 
Amesema,ili kupata huduma hiyo ni vema wakafika katika ofisi zao au kuomba huduma kwa kubonyeza *152*00# na kufuata hatua na sio kufanya mambo wanayoyafanya ambayo yapo nje na utaratibu.
 
Mwenyekiti wa Wakurugenzi wa mgodi huo, James Sita amesema amesikitishwa na kitendo kilichofanywa na baadhi ya wachimbaji wake na kuungana na shirika kuwachukulia hatua za kisheria wachimbaji wote waliobainika.
 
Amesema, nguzo iliyotumika kuchepusha umeme aliileta yeye kwa gharama zake na kuwataka wachimbaji watakaoitumia kupata huduma wafuate utaratibu na siyo kujiunganishia kinyemela na muda wote hakujua kama kuna kitendo cha ubadhirifu kinaendelea.
 
Sita amesema, wanaofanya vitendo hivyo wanasababisha shirika na serikali kukosa mapato yake na wao kupata hasara pale inapotokea tatizo la umeme na kuungaza mitambo yao, na kuwaasa kuacha mara moja tabia hiyo kwani inawachafua na kuonekana watovu wa nidhamu.
















Post a Comment

0 Comments