KAHAMA
Mwenge wa Uhuru umeendelea
kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia katika Halmashauri ya Ushetu,
Wilaya ya Kahama, Mkoa wa Shinyanga, ambapo jumla ya mitungi 50 ya gesi
imegawiwa kwa mama lishe, wakiwemo wanawake wenye ulemavu na wasio na ulemavu.
Hatua hiyo inalenga kuhamasisha
wananchi kuachana na matumizi ya nishati zinazochafua mazingira, hususan kuni
na mkaa, na kuhamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa ajili ya
kulinda afya, mazingira na kupunguza gharama za uendeshaji wa shughuli za kila
siku.
Mmoja wa wanufaika, Eva Maziku kutoka Kata ya
Kinamapula, amesema kupatiwa jiko la gesi kutamsaidia kupunguza gharama za
kununua mkaa huku akilinda afya na mazingira.
Amesema awali alikuwa akitumia
hadi gunia moja la mkaa kwa wiki, ambalo katika eneo hilo hugharimu kati ya
Shilingi 25,000 hadi 30,000.
“Kwa kupata majiko haya, nitakuwa
tayari nimetunza mazingira, na pia nitakuwa nimelinda afya yangu na kuokoa
maisha yangu mimi kama mama. Ninamshukuru sana mama Samia kwa kutuona hata sisi
akina mama lishe wa Ushetu, abarikiwe sana” Amesema Maziku
Kwa upande wake, Lucia Shija, mama lishe
mwenye ulemavu wa viungo, amesema matumizi ya gesi yatamuepusha na changamoto
ya kutafuta kuni porini, jambo ambalo kwake lilikuwa gumu kutokana na hali yake
ya ulemavu.
Amesema hatua hiyo pia itasaidia
kupunguza uharibifu wa mazingira unaotokana na ukataji wa miti kwa ajili ya
kuni.
Amesema “Tunamshukuru Rais Samia
kwa kutuona sisi wenye ulemavu, mimi nilikuwa natumia kuni kwa kukata kwenye
mapori huko, na macho yanakuwa mekundu unaitwa mchawi, lakini sasa hivi
nitapika vizuri.”
Mratibu wa Nishati Safi wa
Halmashauri ya Ushetu, Naomi Ndelwa, amesema Halmashauri hiyo imejipanga
kuendelea kutoa elimu kwa wananchi katika kata zote 20 na vijiji vyake kuhusu
umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Amesema hatua hiyo ni kuunga mkono
jitihada za serikali katika kuhamasisha matumizi ya nishati safipikia kwa
wananchi na kuendelea kulinda misitu na mapori ya akiba yaliyopo katika
halmashauri hiyo.
Amesema kati ya mitungi 50
iliyogawiwa, mitungi 25
imenunuliwa kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri, huku mitungi 30 ikitolewa na wadau
wanaoshirikiana na Halmashauri katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya
kupikia.
“Sisi kama Halmashauri tumejipanga
kutoa elimu kwenye kata zote 20 na vijiji vyake, kuhusu umuhimu wa matumizi ya
nishati safi ya kupikia kwa jamii nzima.” Amesem Mbelwa
Kwa upande wake, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa
mwaka 2026, Wazo Michael Mwang’onda, amewataka wananchi
kuendelea kulinda amani na utulivu nchini, akisisitiza kuwa mazingira ya amani
ndiyo msingi wa kuendelea kupatikana kwa maendeleo.
Amewataka wananchi kuendelea
kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan,
huku akisisitiza umuhimu wa watanzania kushirikiana katika kulinda amani na
utulivu wa nchi.
Amesema “Tulindeni amani na utulivu,
nchi yetu iendelee kubaki na utulivu, tumuombee Rais wetu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dk Samia Suluhu Hassan nay eye ataendelea kutuletea
maendeleo makubwa zaidi.”








0 Comments