Mkuu wa kanda ya ziwa wa Tume ya Taifa ya mpango wa matumizi ya ardhi John Chuwa, akizungumza na wajumbe wa serikali ya kijiji cha Nata, Halmashauri ya Msalala mkoani Shinyanga, wakati akiutambulisha mpango wa matumizi ya ardhi unaotarajiwa kuwafikia zaidi ya wakazi 800 wa vijiji tisa vilivyopitiwa na mradi huo halmashauri ya Msalala mkoani Shinyanga.
Na Mwandishi Wetu - Msalala, Kahama
Vijiji tisa vya Halmashauri ya Msalala wilayani Kahama mkoani Shinyanga, vinatarajiwa kunufaika na uandaaji wa mipango ya matumizi ya Ardhi ikiwa ni jitihada za serikali kuhakikisha ardhi inatumika kuimarisha maendeleo endelevu ya jamii za vijijini.
Hata hivyo, Serikali kupitia wizara ya Ardhi nyumba na maendeleo ya makazi (Tume ya Taifa ya mipango ya matumizi ya Ardhi) imelenga kuendeleza jitihada za kupunguza migogoro ya ardhi nchini, kwa kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi pamoja na kuyamilikisha kwa wananchi.
Mkuu wa kanda ya ziwa wa Tume ya Taifa ya mpango wa matumizi ya ardhi John Chuwa amesema, vijiji hivyo tisa vya Msalala ni miongoni mwa vijiji 23 nchini vinavyopitiwa na mradi wa mpango wa matumizi ya ardhi, huku hati za kimila 6,000 zikitarajia kutolewankatika vijiji vinane.
Chuwa amesema mpango huo utawezesha kutenga maeneo mengine ya matumizi, kupunguza migogoro ya ardhi na kusaidia upatikanaji wa hati miliki za kimila kwa wananchi wa vijijini.
“Tunataka tuandae mipango ya matumizi ya ardhi ambayo itawawezesha wananchi hawa kuendelea na shughuli ya uandaaji wa hati za kimila ili wawe na uhakika wa milki zao, na kutumia hati hizo kwa matumizi mbalimbali.” Amesema Chuwa
Na kuongeza “Kata ya Mwanase imepewa kipaumbele kutokana na kuwa na migogoro mingi ya ardhi ikiwemo mipaka na ukizingatia mpango huu umelenga kutatua migogoro ya vijiji na vijiji lakini pia ya kimatumizi. Wilayah ii ilibaki nyuma katika uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi na sasa serikali imewekeza nguvu kwenye hivi vijiji tisa.”
Amesema katika siku ya kwanza, mpango huo umetambulishwa kwa wananchi ambao wanao wajibu wa kuelewa maeneo yaliyopanga kwa matumizi mbalimbali na kuyasimamia ili yaendelezwe.
Akiwa katika kijiji cha Mwamandi Afisa Mipango Miji kutoka Tume ya Taifa ya Mpango wa Matumizi ya Ardhi Abdallah Magombana, amesema kijiji cha Mwamandi ni moja ya vijiji vilivyokuwa na mgogoro wa mpaka na kijiji cha Nata, lakini kupitia mpango huo kila kijiji kitaweza kujitegemea na kufanya shughuli za maendeleo.
“Halmashauri ina shughuli nyingi za kiuchumi hususani mifugo na kilimo, kwa hiyo kukamilika kwa zoezi hili itakuwa nafasi muafaka kwa wanakijiji kuishi kwa amani na kufanya shughuli zao za kiuchumi bila kuwa na migogoro ya ardhi.” Amesema na kuongeza
“Wananchi wanao wajibu wa kupendekeza kile kitakachokuwa na manufaa kwao na yakafanyiwa kazi na Tume hii kwa kushirikiana na mamlaka ya upangaji ya Halmashauri ya Msalala.”
Kwa upande wake mkuu wa Idara ya Ardhi Halmashauri ya Msalala Danford Mashiba, amesema wamepokea mpango huo na wanatarajia kuwafikia wananchi zaidi ya 800 kutoka katika vijiji hivyo tisa.
Amevitaja vijiji hivyo kuwa ni pamoja na Mwazimba, Kashishi, Mwanase, Mwakuzuka, Mwamandi, Kabondo, Nata, Nyamididi na Umbogo.
Amesema “Halmashauri ya Msalala tunashukuru sana kwa mpango huu. Katika kuutekeleza tunashirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo wananchi wenyewe na idara nyingine kama kilimo, madini, mifugo na uvuvi.”
Diwani wa kata ya Mwanase Joshua Sumuni, ameishukuru serikali kwa mpango huo utakaoleta tija ya moja kwa moja kwa wananchi wa vijiji vilivyolengwa.
“Naishukuru sana serikali chini ya Dkt Samia Suluhu Hassan, kwa kutuletea mpango huu utakaokwenda kutusaidia kutatua migogoro mingi iliyokuwa imeshamiri kwenye kata hii ya Mwananse. Sasa tutayajua maeneo ya malisho, makazi, biashara na maeneo ya huduma za umma.” Amesema Sumuni
Mkazi wa kijiji cha Mwamandi kata ya Mwanase Neema Michael amesema “Huu mpango utatusaidia sisi wananchi kumiliki ardhi zetu kwa uhalali, na tukienda kukopa tutakopesheka kwa sababu tunatambulika kisheria.”
Nae Eva Emanuel mkazi wa kijiji cha Nata amesema “Kwa vile tulivyofundishwa hapa leo, niombe serikali iharakishe hizo hati tumilikishwe ardhi, nimeona hii itanisaidia hata kumuwekea dhamana ndugu yangu akiwa amekamatwa polisi.”






















0 Comments