TANGAZO

TANGAZO

SANGU ATAKA HAMASA KUHUBIRI AMANI, MAADILI NA UMOJA KWA MANUFAA JAMII

 

Viongozi wa dini nchini wameaswa kuendelea kuwa nguzo kuu katika kuhubiri amani, upendo, uvumilivu na maadili mema kwa wananchi ili kulinda na kudumisha umoja wa kitaifa ambao ndio msingi mkuu wa maendeleo endelevu ya Tanzania.



Wito huo ulitolewa jijini Mwanza na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu, alipomwakilisha Waziri Mkuu katika ibada maalumu ya kuliombea taifa iliyoandaliwa na taasisi ya Unity of Christian International (UCI) katika Kanisa la KKKT Dayosisi ya Mashariki ya Ziwa Victoria.

Katika hotuba yake, Waziri Sangu alibainisha kuwa serikali inathamini kwa dhati mchango mkubwa unaotolewa na viongozi wa kiroho, akisisitiza kuwa maendeleo ya kweli ya kiuchumi na kijamii hayawezi kupatikana bila uwepo wa utulivu na mshikamano thabiti miongoni mwa wananchi.

Waziri Sangu alisema Serikali itaendeleza ushirikiano wake wa karibu na taasisi zote za dini pamoja na wadau mbalimbali ili kuhakikisha Tanzania inabaki kuwa kisiwa cha amani na utulivu.

Taasisi hizi zimekuwa na mchango usiopimika katika kujenga jamii inayozingatia uzalendo, uwajibikaji, na maadili, mambo ambayo ni nguzo muhimu katika kufanikisha malengo makubwa ya maendeleo ya taifa.

Kutokana na hilo, viongozi wa kidini wamehimizwa kuelekeza nguvu zao zaidi katika kuwalea vijana kiadili na kuwahamasisha kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji, kwa kuwa kundi hilo ndilo linalobeba nguvu kazi na hatari ya mustakabali wa baadae wa nchi yetu.

Katika kuelekea utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050, ushirikiano wa karibu kati ya mamlaka za kiserikali na sekta ya dini unatajwa kuwa chachu ya mafanikio.

Viongozi wa kidini, wakiongozwa na Askofu Kiongozi wa UCI, Wilson Munguza, wameonyesha utayari wao wa kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali kwa kuomba na kuhamasisha utu na mshikamano katika jamii.

Kupitia misingi hii ya kiroho na kimaadili, jamii inapata mwelekeo sahihi unaosaidia kupunguza uhalifu, kuongeza uwajibikaji kazini, na kujenga mazingira salama na tulivu yanayomwezesha kila mwananchi kuchangia kikamilifu katika ustawi wa taifa zima.

Post a Comment

0 Comments