TANGAZO

TANGAZO

NSSF NA ATE WASAINI MKATABA WA USHIRIKIANO KUIMARISHA HUDUMA NA USTAWI WA WAFANYAKAZI

 




Na MWANDISHI WETU,


Dar es Salaam.

Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) tarehe 25 Juni, 2026 wamesaini mkataba wa ushirikiano wenye lengo la kuimarisha mahusiano ya kikazi, kubadilishana taarifa na uzoefu, pamoja na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya taasisi hizo kwa manufaa ya waajiri, wafanyakazi na taifa kwa ujumla.

Mkataba huo ulisainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba, na Mtendaji Mkuu wa ATE, Bi. Suzanne Ndomba-Doran, katika hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam, mbele ya Mgeni Rasmi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Mhe. Deus Sangu, sambamba na Mkutano Mkuu wa 67 wa ATE.

Kupitia makubaliano hayo, NSSF na ATE watashirikiana katika kujengeana uwezo, kubadilishana utaalamu na ujuzi, kuendesha programu za elimu kwa wadau, pamoja na kuimarisha mazingira bora ya kazi na hifadhi ya jamii nchini.

Ushirikiano huo unaakisi dhamira ya pamoja ya taasisi hizo katika kuendeleza huduma bora na kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya Tanzania.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Deus Sangu aliwataka waajiri nchini kutumia fursa ya msamaha wa tozo iliyotolewa na NSSF kwa waajiri wenye malimbikizo ya michango ya wanachama kwa kuhakikisha wanakamilisha malipo yao ndani ya kipindi kilichowekwa.

Alisema msamaha huo, ulioombwa na waajiri kupitia ATE, unaonesha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuendelea kujenga mazingira wezeshi ya biashara, kazi na uwekezaji kwa kusikiliza na kutatua changamoto za wadau mbalimbali wa maendeleo. Aidha, alisema Serikali itaendelea kuimarisha mfumo wa kazi, ajira na hifadhi ya jamii ili kukuza uchumi jumuishi na ustawi wa wananchi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba, alisema msamaha wa tozo ulioanza kutekelezwa Juni 1, 2026 na utakaoendelea hadi Desemba 31, 2026 utawapa waajiri nafuu ya kifedha na kuwawezesha kuelekeza rasilimali zaidi katika uzalishaji, ukuaji wa biashara na uundaji wa ajira.

Alisema kupitia msamaha huo, mwajiri atakayelipa deni lake kabla ya tarehe 31 Agosti 2026 atasamehewa asilimia 100 ya tozo, atakayelipa kabla ya tarehe 31 Oktoba 2026 atasamehewa asilimia 75, na atakayelipa kabla ya tarehe 31 Desemba 2026 atasamehewa asilimia 50. Aidha, mwajiri ambaye amekuwa akiwasilisha na kulipa michango yake kwa wakati bila malimbikizo tangu mwezi Mei 2026 atasamehewa asilimia 100 ya tozo.

Bw. Mshomba aliongeza kuwa ushirikiano kati ya NSSF na ATE utaimarisha utoaji wa elimu ya hifadhi ya jamii na kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa mifumo ya kinga ya kijamii kwa waajiri na wafanyakazi.

Naye Mtendaji Mkuu wa ATE, Bi. Suzanne Ndomba-Doran, alisema mfumo imara wa hifadhi ya jamii ni nyenzo muhimu katika kujenga nguvu kazi yenye tija na ushindani, huku ukiendelea kuimarisha mazingira bora ya biashara na kuchangia ukuaji endelevu wa uchumi wa taifa.




Post a Comment

0 Comments