

📍KAHAMA
Katika kuadhimisha miaka 30 ya mamlaka ya mapato Tanzania (TRA), Mamlaka
hiyo katika Mkoa wa Kikodi Kahama, imevuka lengo la makusanyo ya mwaka wa fedha
2025/2026 kwa kukusanya zaidi ya Shilingi bilioni 44, sawa na
zaidi ya asilimia 120 ya lengo la Shilingi bilioni 35.
TRA mkoa wa Kahama unaadhimisha miongo hiyo mitatu kwa shughuli
mbalimbali zilizohusisha walipa kodi waliopo sambamba na
kuwatengeneza wapya, ikiwemo mazoezi ya pamoja (jogging) pamoja na upandaji wa
miti.
Meneja wa TRA mkoa wa Kahama, Wisaka Kamwamu, akizungumza mara baada ya kumalizika kwa shughuli ya jogging, ametaja chanzo cha mafanikio hayo kuwa ni pamoja na ushirikiano mzuri
kati ya TRA, walipa kodi na viongozi wa serikali kupitia ofisi ya mkuu wa
wilaya ya Kahama.
Jogging hiyo iliyowakutanisha
watumishi wa TRA, walipa kodi na wadau mbalimbali wa michezo, wakiwemo Kahama
Jogging Club, Kamwamu
amesema tukio hilo limelenga kuwapongeza walipa kodi kwa mchango wao katika
maendeleo ya Taifa na kuimarisha uhusiano kati ya TRA na wadau wake.
Amesema tangu kuanzishwa kwa TRA, taasisi hiyo imeendelea kupitia
hatua mbalimbali za maboresho, huku kipindi cha miaka ya hivi karibuni
kikishuhudia ongezeko kubwa la makusanyo katika Mkoa wa Kahama.
Amesema "Lengo letu la siku hii ni kutambua mchango wa walipa
kodi wetu, na namna ambavyo tumeshirikiana nao katika hatua mbalimbali za
kikodi. Ushirikiano huu umetupa mafanikio makubwa kwenye makusanyo.”
Amesema mwitikio
mkubwa wa wafanyabiashara, wanamichezo na wananchi katika jogging hiyo,
umeongeza hamasa kwa watumishi wa TRA na walipa kodi, jambo litakaloendelea
kuimarisha uhusiano na kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato.
Kwa mujibu wa Kamwamu, katika mwaka wa fedha unaomalizika, TRA
Kahama ilipangiwa kukusanya Shilingi bilioni 35, lakini
hadi sasa imefanikiwa kukusanya zaidi ya Shilingi bilioni 44, ikiwa ni
ongezeko la zaidi ya Shilingi bilioni 9.
Amesema hayo ni mafanikio makubwa ambayo yameifanya Kahama
kuendelea kuwa miongoni mwa mikoa inayofanya vizuri katika makusanyo kwa miaka
mitatu mfululizo.
Kamwamu ameeleza kuwa mafanikio hayo yametokana na ushirikiano wa
karibu kati ya watumishi wa TRA, wafanyabiashara, viongozi wa serikali pamoja
na matumizi ya mifumo ya kidijitali, ambayo imerahisisha huduma nyingi za
kikodi bila ulazima wa walipa kodi kufika katika ofisi za TRA.
Aidha, aliwataka wafanyabiashara kuendelea kushirikiana na TRA kwa
kufika katika ofisi zake kila wanapokutana na changamoto ili zipatiwe ufumbuzi
kwa wakati.
"TRA ni chombo cha wananchi. Bila ushirikiano wa walipa kodi
hatuwezi kufikia malengo yetu ya ukusanyaji wa mapato. Tunawaomba waendelee
kushirikiana nasi ili tuendelee kujenga uchumi wa mkoa na taifa kwa
ujumla," ameongeza
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kahama Jogging Club,
Abdallah Mmagane,
amesema ushirikiano kati ya klabu hiyo na TRA umekuwa wa mfano, na umewezesha
wananchi wengi kushiriki mazoezi yanayolenga kuboresha afya na kujikinga dhidi
ya magonjwa yasiyoambukiza.
Amesema Kahama Jogging Club itaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali
za serikali na binafsi, katika kuhamasisha wananchi kufanya mazoezi kwa ajili
ya afya bora.
Naye Afisa Habari wa Kahama Jogging Club, Ketty Rugy, amesema wamewiwa
kushiriki maadhimisho ya miaka 30 ya TRA kwani wanachama wengi wa klabu hiyo ni
wafanyabiashara, huku akiwasihi kuendelea kulipa kodi kwa hiari.
Amesema "Tumeshiriki
wengi kwa sababu wengi wetu ni wafanyabiashara, hivyo tumekuwa tukishirikiana
kwa karibu sana na TRA. Ninawaomba wafanyabiashara wote tuendelee kulipa kodi, bila
kodi hakuna maendeleo ya nchi yetu."
Wakati
huohuo TRA Mkoa wa Kikodi Kahama, imepanda miti
katika Shule ya Sekondari Kishimba ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 30
ya TRA, na kutekeleza wajibu wake kwa jamii (Corporate Social Responsibility),
mara baada ya kumalizika kwa shughuli ya.
Meneja Kamwamu amesema shule hiyo imechaguliwa kwa makusudi kutokana na
nafasi yake ya kulea kizazi kitakachokuwa walipa kodi na wataalamu wa baadaye,
wakiwemo maofisa wa kodi.
Amesema "Tumekuja
Kishimba sekondari kwa sababu tunatambua hapa ndipo wanalelewa vijana wetu.
Hawa ndiyo walipa kodi wa kesho na tunategemea pia kupata maofisa wa kodi. Hii
ni sehemu ya wajibu wetu kwa jamii kama taasisi ya serikali.”
Aliongeza kuwa walimu wa shule hiyo
pia ni walipa kodi wanaochangia mapato ya serikali, hivyo TRA itaendelea
kushirikiana na taasisi za elimu katika kuhamasisha maendeleo na utunzaji wa
mazingira.
Naye Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari
Kishimba, Adelina Massawe, ameishukuru
TRA kwa kuichagua shule hiyo, na kwamba miti hiyo itachangia kuboresha
mazingira ya kujifunzia na kuwajengea wanafunzi utamaduni wa kutunza mazingira.
"Tunawashukuru sana TRA kwa kutuchagua, huu ni ujumbe mzuri kwa wanafunzi wetu kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira. Miti hii itasaidia kuboresha mazingira ya shule na kuwapa wanafunzi sehemu nzuri za kujifunzia na kufanya majadiliano.” Amesema Massawe






















0 Comments