Mkuu wa Kituo hicho Mkaguzi Msaidizi Hafidhi Omari, akitoa elimu ya majanga na maokozi kwa wafanyabiashara wa soko la Majengo katika Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga katika tukio la utayari kwa wafanyabiashara wa soko hilo na askari wa zimamoto.

Na mwandishi wetu - Kahama
Jeshi la zimamoto na uokoaji mkoani Shinyanga, kupitia kituo cha Kahama, limefanya tukio la utayari kwa wananchi na wafanyabiashara wa soko la Majengo Manispaa ya Kahama.
Mkuu wa Kituo hicho Mkaguzi Msaidizi Hafidhi Omari, amesema tukio hilo limelenga kupima utayari na uwezo wa askari wake katika kukabiliana na majanga ya moto na maokozi pindi yanapotokea sambamba na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kukabiliana na majanga ya moto.
Omari amewasihi wananchi kufuata taratibu za ujenzi wa makazi bora ili zinapotokea dharura ikiwemo majanga ya moto kurahisisha maokozi kwa gari kuweza kupita na kufika eneo la tukio kwa wakati.
Amesema “Hili ni tukio la utayari, la kukufanya wewe uwe tayari dhidi ya majanga ya moto na mengineyo, lakini na sisi kama taasisi tuwe tayari pia kupokea taarifa za hayo matukio na kuitikia kwa wakati.”
Na kuongeza “Mmeona moto umewaka hapa, lakini ndani ya dakika chache mno tumefika, tafsiri yake ni nini? Ni utoaji wa taarifa, mwenyekiti ametupa taarifa na sisi tumefika kwa wakati.”
“Tunapopata taarifa kwa wakati, tunafika eneo la tukio kwa wakati. Piga namba 114 ni bure, yanapotokea majanga ya moto na mengine yanayohitaji maokozi. Tuondoe dhana ya kwamba jeshi la zimamoto linachelewa kufika kwenye matukio, kuchelewa kwetu ni vile nyinyi wananchi mtakavyochelewa kutupa taarifa.” Amesisitiza
Aidha ameonya tabia ya baadhi ya watu wanaotumia simu zao za mkononi kuchezea nambari hiyo ya dharura kwa kupiga simu na kutoa taarifa za uongo na kwamba kitendo hicho ni kuwakosesha huduma wenye uhitaji lakini pia matumizi mabaya ya mali za jeshi hilo.
Amesema “Wewe unapochezea hii namba kuna mwenzako anapata dharura ambayo inahitaji kupata huduma ya kweli lakini pia ni kosa kisheria, tunawasihi watu wa Kahama msifanye hivyo.”
Mwenyekiti wa Soko la Majengo, Amani Omari amelishukuru na kulipongeza Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Kahama kwa juhudi wanazozifanya katika kuokoa maisha na mali za wananchi.
Amesema zoezi lililofanyika linaeleza kwa vitendo kwa wananchi nini cha kufanya endapo wakipata majanga ya moto na majanga mengine kwenye maeneo yao jambo ambalo litarahisisha maokozi zinapotokea dharura.
Amesema “Jeshi la zimamoto leo limetuonyesha kwa vitendo namna ya kufanya maokozi kwenye majanga ya moto wakiwemo majeruhi wa moto, tunawashukuru sana kwa zoezi hili, tumejua pia namba yao ya dharura ambayo ni 114 itaturahisishia kutoa taarifa za majanga mbalimbali.

Baadhi ya wafanyabiashara wa soko la Majengo, katika Manispaa ya Kahama, mkoani Shinyanga wakieleza namna ya utoaji wa taarifa kwa jeshi la zimamoto na uokoaji kuhusu taarifa za majanga na maokozi baada ya kupewa elimu hiyo na mkuu wa kituo cha Kahama Mkaguzi Msaidizi Hafidhi Omari.

Askari wa jeshi la zimamoto na uokoaji kituo cha Kahama, mkoani Shinyanga, wakifanya jaribio la maokozi ya majeruhi wa tukio la moto wakati wa tukio la utayari kwa wafanyabiashara wa soko hilo na askari wa zimamoto.

Mwenyekiti wa soko la Majengo Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga Amani Omari (kushoto) akizungumza muda mfupi baada ya kupata elimu ya majanga na maokozi kutoka kwa jeshi la zimamoto na uokoaji Kahama, likiongozwa na mkuu wa kituo hicho Mkaguzi Msaidizi Hafidhi Omari, wakati wa tukio la utayari kwa wafanyabiashara wa soko hilo na kupima utayari wa askari wake.





0 Comments