Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Janeth Magomi.
Na Mapuli Kitina Misalaba
Mfanyakazi wa ndani aitwaye Neema Justine mwenye umri wa Miaka 19, mkazi wa Kata ya Old Shinyanga, amefariki dunia kwa tuhuma za kujinyonga ndani ya nyumba aliyokuwa akiishi, tukio lililotokea majira ya mchana.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Soko B, Kijiji cha Old Shinyanga, Bwana Leonardo Magige amesema alipokea taarifa za tukio hilo majira ya saa sita mchana na kufika haraka eneo la tukio kwa ajili ya kufuatilia kilichotokea.
Amesema kwa mujibu wa maelezo ya familia, siku ya tukio mama mwenye nyumba alikuwa akifanya shughuli za kufua nguo asubuhi, ambapo baadaye mfanyakazi huyo wa ndani naye alieleza kuwa ana nguo zake za kufua. Hata hivyo, mama huyo aliamua kufua nguo hizo kabla ya kuondoka kwenda kazini.
Kabla ya kuondoka, mama huyo aliondoka na mtoto wake kwenda kazini kwake (dukani) ambapo alimpatia mtoto wake hela kwa ajili ya kununua mahitaji ya chakula, na aliporudi nyumbani alimkuta Neema akiwa tayari amefariki kwa kujinyonga dirishani bila kuacha ujumbe wowote.
“Baada ya kupata taarifa hizo, niliwasiliana na polisi wa kata ambao nao walitoa taarifa kituo cha polisi. Maafisa walifika eneo la tukio na kuchukua mwili wa marehemu kuupeleka katika Hospitali ya Manispaa ya Shinyanga kwa uchunguzi zaidi,” amesema Magige.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Janeth Magomi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema uchunguzi unaendelea ili kubaini chanzo chake.
“Tulipokea taarifa kutoka kwa Evaline Richard aliyegundua kifo cha mfanyakazi wake wa ndani, Neema Justine, ambaye alifariki kwa kujinyonga ndani ya nyumba aliyokuwa akiishi. Hadi sasa chanzo hakijajulikana kwani hakukuwa na ujumbe wowote ulioachwa,” amesema Kamanda Magomi.
SACP Magomi ametoa wito kwa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kuimarisha malezi na mawasiliano ndani ya familia, pamoja na kuwachukulia wafanyakazi wa ndani kama sehemu ya familia ili kuwapa mazingira salama ya kuishi.
Naye Mwenyekiti wa Kitongoji, Magige, amesisitiza umuhimu wa wazazi kuwa karibu na watoto wao ili waweze kueleza changamoto wanazokutana nazo bila hofu.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Manispaa ya Shinyanga, huku jeshi la polisi likiendelea na uchunguzi wa tukio hilo.
Tukio hili linakuja ikiwa ni tukio la pili la aina hiyo kuripotiwa katika Kata ya Old Shinyanga katika kipindi cha hivi karibuni ambapo mwanafunzi wa kidato cha Nne alifariki kwa kujinyonga.
0 Comments