TANGAZO

TANGAZO

WIKI YA ZIMAMOTO DUNIANI: ZIMAMOTO KAHAMA YAVIFIKIA VILABU VYA WANAFUNZI MASHULENI

 


Mkuu wa kituo cha jeshi la zimamoto na uokoaji wilayani Kahama mkoani Shinyanga mkaguzi msaidizi Hafidhi Omari (kulia), akitoa elimu ya majanga na maokozi kwa club ya zimamoto shule ya msingi Igomelo, Manispaa ya Kahama katika kuadhimisha wiki ya zimamoto duniani, wilayani humo.

Katika kuadhimisha Wiki ya Zimamoto Duniani, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wilaya ya Kahama kupitia Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma, limetembelea Shule ya Sekondari Kishimba na Shule ya Msingi Igomelo, kwa lengo la kutoa elimu ya kinga na tahadhari dhidi ya majanga kwa wanafunzi.

 

Elimu hiyo imetolewa kupitia vilabu vya zimamoto vilivyopo mashuleni(Fire clubs), ikiwa na lengo la kuwawezesha wanafunzi kuwa mabalozi wa usalama kwa wenzao na hata wazazi wao majumbani.

 

Akizungumza katika ziara hiyo, Mkuu wa Kituo cha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wilaya ya Kahama, Mkaguzi Msaidizi Hafidhi Omari, amesema kuwa utoaji wa elimu hiyo ni sehemu ya juhudi za jeshi hilo, kuhakikisha jamii inakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu namna ya kukabiliana na majanga na utoaji wa taarifa.

 

Amesisitiza umuhimu wa kutoa taarifa kwa wakati pindi majanga yanapotokea, akiwahimiza wanafunzi na walimu kutumia namba ya dharura 114 ili kuwezesha jeshi hilo kufika haraka katika maeneo ya tukio.

 

“Tunatumia Wiki ya Zimamoto Duniani kuwafikia wanafunzi kupitia vilabu vyao ili waweze kuelewa wajibu wao katika kuzuia na kuripoti majanga. Wito wetu ni kutoa taarifa mapema kupitia namba 114 ili kupunguza madhara zaidi kwa watu na mali.” amesema Omari na kuongeza

 

“Huu ni muendelezo wa elimu ambayo tumekuwa tukiitoa mara kwa mara kupitia vilabu hivi, lakini katika kuadhimisha wiki hii ya zimamoto duniani, tumeona tuvifikie tena ili kuvijengea uwezo na tunaamini kupitia watoto hawa elimu inaenda mbali zaidi.”



Mkuu wa kituo cha jeshi la zimamoto na uokoaji wilayani Kahama mkoani Shinyanga mkaguzi msaidizi Hafidhi Omari (kulia), akitoa elimu ya matumizi ya nambari ya dharura ya jeshi hilo endapo yakitokea majanga kwa wanafunzi na walimu ya shule ya msingi Igomelo, Manispaa ya Kahama katika kuadhimisha wiki ya zimamoto duniani, wilayani humo.

 *******

Walimu na wanafunzi katika shule hizo, wameipongeza Zimamoto Kahama kwa kuwapatia elimu hiyo muhimu, wakisema itawasaidia kuongeza uelewa wa tahadhari na kuchukua hatua stahiki wakati wa dharura.

 

Jeshi la Zimamoto na Uokoaji linaendelea kutumia maadhimisho ya Wiki ya Zimamoto Duniani, kama fursa ya kutoa elimu kwa jamii, ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kupunguza athari za majanga na kuokoa maisha pamoja na mali za wananchi.


Mkuu wa kituo cha jeshi la zimamoto na uokoaji wilayani Kahama mkoani Shinyanga mkaguzi msaidizi Hafidhi Omari, akisaini kitabu cha wageni katika shule ya sekondari Kishimba Manispaa ya Kahama, alipofika pamoja na askari wa jeshi hilo kwa ajili ya kutoa elimu kwa walimu pamoja na wanafunzi kupitia club ya zimamoto shuleni hapo katika kuadhimisha wiki ya zimamoto duniani, wilayani humo.



Mkuu wa kituo cha jeshi la zimamoto na uokoaji wilayani Kahama mkoani Shinyanga mkaguzi msaidizi Hafidhi Omari, akisaini kitabu cha wageni katika shule ya msingi Igomelo Manispaa ya Kahama, alipofika pamoja na askari wa jeshi hilo kwa ajili ya kutoa elimu kwa walimu pamoja na wanafunzi kupitia club ya zimamoto shuleni hapo katika kuadhimisha wiki ya zimamoto duniani, wilayani humo.

Post a Comment

0 Comments