Na Mwandishi Watu,Dar es Salaam
Wananchi wa Mkoa wa Dar Es Salaam wamesema kuundwa kwa Tume huru ya uchunguzi wa matukio ya Uvunjifu wa amani yaliyotokea wakati na baada ya uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 lilikuwa tukio la kiungwana na la kuungwa Mkono na Kila Mtanzania, wakieleza matarajio yao kwamba ripoti ya Tume hiyo itakayokabidhiwa hivi karibuni kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itadumisha amani ya nchi na kudhibiti matukio ya uvunjifu wa amani nchini.
Kauli hiyo imetolewa na baadhi ya wananchi wa Ilala Mkoani Dar Es Salaam leo Jumamosi Aprili 04, 2026 wakati wakizungumza na waandishi wa habari kuhusu matarajio yao wakati huu ambapo Tume hiyo iktarajiwa kukabidhi ripoti yake kwa Rais Samia, wakimpongeza pia Rais Samia kwa utashi wake wa kuamua kuunda tume hiyo.
"Nimpongeze sana Mhe. Rais Samia kwa kuunda Tume hii na ni dhihirisho la kuitakia mema nchi pamoja na Watanzania wote, angekuwa hatutakii mema angeweza kukaa kimya na hakuna ambacho tungemfanya." Amesema Bw. Mohammed Bohero, Mkazi wa Karume Jijini Dar Es Salaam.
Kwa upande wake Bw. Jamal Sadat Mbiku, ameeleza matarajio yake katika ripoti hiyo akibainisha kuwa matokeo ya ripoti hiyo yatakuwa suluhu ya kudumu dhidi ya matukio mengine kama yaliyotokea Oktoba mwaka jana sambamba na kuwa nyenzo muhimu itakayoendeleza na kudumisha amani iliyopo nchini.
Wakati akizindua Tume hiyo, Rais Samia aliitaka kuchunguza madai ya Vijana kutaka haki, kuangalia sababu ya Vijana kuingia barabarani na kufanya matukio ya uvunjifu wa amani sambamba na kuangalia matamshi ya Vyama vya siasa ambavyo baadhi yake viliahidi kuzuia uchaguzi pamoja na kuangalia mahusiano ya Vyama hivyo vya siasa na Tume huru ya Taifa ya uchaguzi (INEC) pamoja na ushiriki wa Vyama na Mashirika Binafsi walivyojihusisha na matukio hayo ya uvunjifu wa amani.
Tume hiyo inaongozwa na Mwenyekiti wake Jaji Mkuu mstaafu Mohamed Chande Othman, akiwa ni Kiongozi mwenye uzoefu katika tasnia ya sheria, utoaji wa haki na masuala ya haki za binadamu Kitaifa na Kimataifa, akifahamika na kuheshimika kutokana na uelewa na uzoefu wake mkubwa katika sekta ya sheria na siasa za Kimataifa


0 Comments