Kuelekea maadhimisho ya Siku ya Zimamoto Duniani, Jeshi la zimamoto na uokoaji wilayani Kahama mkoani Shinyanga limeshiriki katika shughuli ya upandaji miti ikiwa ni sehemu ya kushiriki utunzaji wa mazingira na kurejesha uoto wa asili.
Akizungumza wakati wa shughuli hiyo iliyofanyika kwenye ofisi za zimamoto Kahama, Mkuu wa Kituo cha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Wilaya ya Kahama Mkoa wa Shinyanga, mkaguzi msaidizi Hafidhi Omari amesema, wamefikia uamuzi huo kutokana na mchango mkubwa wa miti katika uhifadhi wa mazingira.
Amesema “Tumeshiriki zoezi hili kutokana na faida kubwa za miti kwenye maisha yetu ya kila siku ikiwemo, kuzuia mmomonyoko wa udongo na ukame, kuongeza uoto wa asili na hifadhi za misitu, kulinda vyanzo vya maji na kusaidia kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.”
Aidha amehimiza jamii kuendelea kushiriki kikamilifu katika upandaji na utunzaji wa miti ili kuhakikisha mazingira yanabaki salama kwa kizazi cha sasa na kijacho.
ELIMU.
Sambamba na zoezi hilo, jeshi la zimamoto na uokoaji Kahama kupitia kitengo cha mawasiliano na uhusiano kwa umma, katika kuelekea wiki ya zimamoto, limeendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu kinga na tahadhari za majanga ya moto, hususani hatari ya kuchota mafuta kutoka kwenye magari yanayopata ajali kwenye maeneo yao.
Akizungumza na wananchi na wafanyabiashara wa kituo cha mabasi CDT na Bukondamoyo Manispaa ya Kahama, Omari amesema elimu hiyo inalenga kuongeza uelewa kwa jamii juu ya tahadhari zinazopaswa kuchukuliwa ili kuepusha ajali za moto majumbani, kazini na katika maeneo ya umma.
Amewataka wananchi kuepuka kukimbilia kuchota mafuta inapotokea ajali, kwani ni hatari na kunaweza kusababisha mlipuko na moto unaoweza kusababisha madhara kwa binadamu na mali.
“Msikimbilie kuchota mafuta pale magari ya mafuta yanapopata ajali, kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza ikiwemo mlipuko endapo kutatokea chanzo cha joto, mfano uvutaji wa sigara, msuguano wa vyuma na shoti kwenye mfumo wa umeme wa gari.” Amesema Omari
Na kuongeza “Pia cheche zinazosababishwa na mgusano wa terminal kwenye battery ama kuwasha viberiti. Ni vyema wananchi wakajiepusha na uchotaji wa mafuta kwa usalama wao na vyombo vingine.”
Amesema elimu hiyo ni sehemu ya juhudi za jeshi hilo kuimarisha uelewa wa jamii kuhusu usalama na namna ya kuepuka madhara yanayoweza kuzuilika hususani katika kuadhimisha wiki ya zimamoto.
Amewahimiza wananchi kutoa taarifa kwa wakati pale wanapoona dalili za moto au tukio la ajali kwa kupiga namba ya dharura 114, ili kuwezesha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kufika kwa haraka na kuchukua hatua stahiki.
Aidha, wananchi wamehimizwa kushiriki kikamilifu katika maadhimisho hayo, kwa kujifunza namna bora ya kutumia vifaa vya kuzimia moto, kutoa taarifa kwa haraka panapotokea dharura, na kufuata maelekezo ya wataalamu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.
Maadhimisho haya yanayotarajiwa kufikia kilele Mei 04, 2026, pia yanatoa fursa ya kutambua mchango wa askari wa zimamoto katika kulinda maisha na mali za wananchi.
Amesema “Tunaendelea kutoa wito kwa wananchi wote kuzingatia maelekezo ya usalama yanayotolewa mara kwa mara, ili kujilinda dhidi ya majanga ya moto na kuchangia katika kuimarisha usalama wa jamii kwa ujumla.”
Askari wa kituo cha jeshi la zimamoto na uokoaji wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga CPL Melania Masika, akipanda mti mapema leo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya Zimamoto Duniani, wilayani humo.
Hata hivyo jamii inakumbushwa kupiga namba 114 bure kabisa, kutoa taarifa za maokozi ikiwemo majanga ya moto haraka zaidi kwa jeshi hilo ili kurahisha shughuli ya maokozi.
Aidha angalizo ni kwa baadhi ya wananchi kuacha mara moja kuchezea/kudhihaki nambari 114 kwa kutoa taarifa za uongo, ili kutoa nafasi kwa wenye majanga kupewa huduma, lakini pia kuepusha hasara na gharama zisizo za lazima kwa jeshi hilo. Hatua za kisheria zitachukuliwa kwa watakaobainika kufanya udanganyifu wowote.
.jpeg)




0 Comments