Viongozi wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu na wa halmashauri ya wilaya ya Nyang’wale wakikabidhiana vifaa kwa ajili ya usafi kwenye halmashauri ya wilaya ya Nyang'wale mkoani Geita, kupitia fedha za uwajibikaji kwa jamii (CSR), muda mfupi baada ya hafla ya makabidhiano ya trekta lenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 66.Nyang'wale - Geita
Mgodi wa Barrick Bulyanhulu umeendelea kutekeleza sera yake ya mkakati endelevu wa kusaidia jamii kupitia fedha za uwajibikaji kwa jamii (CSR), kwa kukabidhi trekta la kusombea taka, lenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 66, pamoja na vifaa vya kufanyia usafi kwa Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’wale mkoani Geita, ikiwa ni juhudi za mgodi kuendeleza utunzaji wa mazingira nchini.
Akizungumza katika hafla ya kupokea trekta hilo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Nyang'wale ,Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo John Isack amesema trekta hilo limekuja kwa wakati, katika juhudi za kulinda na kutunza mazingira kwa maslahi ya wakazi wa wilaya hiyo na vitongoji vyake.
Amesema "Tunashukuru Barrick Bulyanhulu kwa Msaada huu wa trekta , tunaamini sasa hali ya usafi katika Wilaya yetu itakuwa nzuri kwa kiasi kikubwa kwani hili ni trekta la pili wametupatia.
Na kuongeza "Matarajio yetu ni kuongeza kasi ya Kuondoa taka kutoka awali ya kutoa mara mbili kwa wiki, yaani Alhamisi na Jumatatu hivyo tutaongeza siku. Pia tunatarajia kuongeza huduma kwa maeneo ya miji yanayokuwa kwa kasi kibiashara kama vile Bosolwa, Nyijundu, Bukwimba na Maeneo ya migodini."
Isack Amengeza kuwa Barrick Bulyanhulu kupitia uwekezaji wake, imefanikisha miradi mingi ya kijamii na utunzaji wa mazingira wilayani humo, kupitia fedha za Uwajibikaji kwa jamii (CSR) ambayo inazidi kuboresha maisha ya wananchi, na kusisitiza kuwa ni kampuni ambayo ni mfano wa kuigwa.
“Leo tumepokea Trekta ambalo limenunuliwa na kampuni ya Barrick Bulyanhulu kwa gharama ya Shilingi 66 Milioni, Trekta hili ni maalum kwa kazi ya kuzoa uchafu na kupeleka dampo kwa kweli ni msaada mkubwa kwa wilaya yetu kwani kwa miaka mingi sana tumekuwa na changamoto juu ya uzoaji wa taka katika mitaa yetu ukichukulia kwamba mji wetu unakua kwa kasi na kupelekea uzalishaji wa taka kuongezeka kwa kasi, na ni matarajio yangu sasa mazingira ya Wilaya yetu yatakuwa safi, nichukue fursa hii kuwaomba wananchi kufanya usafi kila siku kwani tayari kwa sasa tunalo trekta ambalo litakuwa linasomba taka mara kwa mara”, alisema.
Afisa Mwandamizi wa Idara ya Mahusiano kwa Jamii katika Mgodi wa Barrick Bulyanhulu Zuwena Senkondo, ametoa shukrani kwa viongozi wa serikali na wananchi kwa kuwa na uhusiano mzuri na Kampuni hiyo, na kuongeza kuwa msaada wa trekta lililokabidhiwa ni kwa ajili ya kufanya usafi na utunzaji wa mazingira.
“Niwaombe ndugu zangu usafi ni jukumu letu sote,trekta hili tulitunze ili liweze kuboresha mazingira yetu ipasavyo, milioni 66 ni pesa nyingi hivyo naamini tutakuwa tumefungua njia ya kuboresha mazingira ya usafi wilayani Nyang’hwale, haswa ikizingatia kampuni ya Barrick Bulyanhulu ni wadau wakubwa wa utunzaji wa mazingira”, alisisitiza Zuwena
Afisa Mwandamizi wa Idara ya Mahusiano kwa Jamii katika Mgodi wa Barrick Bulyanhulu, Zuwena Senkondo (Kulia) akipeana mkono wa shukrani na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyang'wale John Isack mara baada ya makabidhiano ya Trekta kwa ajili ya kusomba taka na kufanya usafi kwenye manispaa hiyo.Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyang'wale John Isack (kushoto) wakipokezana na Afisa Mwandamizi wa Idara ya Mahusiano kwa Jamii katika Mgodi wa Barrick Bulyanhulu, Zuwena Senkondo mara baada ya halfa ya makabidhiano ya Trekta kwa ajili ya usafi kwenye halmashauri hiyo .Afisa Mwandamizi wa Idara ya Mahusiano kwa Jamii katika Mgodi wa Barrick Bulyanhulu, Zuwena Senkondo akizungumza kwenye halfa ya makabidhiano ya trekta lenye thamani ya Shilingi milioni 66 lililotolewa na mgodi kwa halmashauri ya Nyang’wale kwa ajili ya usafi wa mazingira.





0 Comments