TANGAZO

TANGAZO

MKUU WA MKOA WA IRINGA KHERI JAMES AFUNGUA KONGAMANO LA WADAU WA HABARI, AIPONGEZA MISA TAN KWA KUIMARISHA WELEDI WA VYOMBO VYA HABARI

  

Na Mapuli Kitina Misalaba

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Kheri James, amesema uwepo wa wahariri na waandishi wa habari kutoka maeneo mbalimbali ya nchi unaonesha umuhimu mkubwa wa sekta ya habari katika kujenga taifa lenye uwazi, uwajibikaji na maendeleo endelevu, huku akisisitiza kuwa vyombo vya habari vina jukumu la msingi la kuhabarisha, kuelimisha na kuchochea mjadala wa maendeleo katika jamii.



Kauli hiyo ameitoa leo Machi 17, 2026 wakati akifungua rasmi Mkutano wa Wahariri na Waandishi wa Habari kutoka Tanzania Bara na Zanzibar ulioandaliwa na Media Institute of Southern Africa (MISA), uliofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa.

Amesema uwepo wa wadau hao wa habari ni muhimu katika kuimarisha misingi ya uwazi na uwajibikaji katika jamii, akibainisha kuwa sekta ya habari ina nafasi kubwa katika kuathiri fikra na mwelekeo wa maendeleo ya taifa.

Mhe. James ametumia fursa hiyo kuwakaribisha washiriki wote mkoani Iringa, akieleza kuwa mkoa huo una mazingira rafiki ya uwekezaji na rasilimali nyingi zikiwemo kilimo, mifugo, misitu na utalii, huku akisisitiza kuwa uchumi wake unaendelea kukua kwa kasi.

Aidha, amesema Serikali imeendelea kuwekeza katika miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo afya, elimu, miundombinu ya barabara, maji, nishati na utalii, hali inayochochea ukuaji wa uchumi na kuboresha maisha ya wananchi. Amebainisha kuwa sekta ya kilimo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wa mkoa huo.

Katika sekta ya utalii, amesema Mkoa wa Iringa una vivutio muhimu kama Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, Udzungwa pamoja na maeneo ya kihistoria kama Kalenga, na kuutaja kuwa kitovu cha utalii katika ukanda wa kusini mwa Tanzania.

Kwa upande wa miundombinu, amesema Serikali imeendelea kuboresha barabara, huduma za umeme na maji pamoja na usafiri wa anga kupitia uboreshaji wa Uwanja wa Ndege wa Nduli ili kufungua fursa zaidi za biashara na uwekezaji.


Amewataka waandishi wa habari kutumia kalamu zao kuitangaza Iringa na Tanzania kwa ujumla ili kuvutia wawekezaji na watalii pamoja na kuchochea maendeleo ya taifa.


Pia amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi za Serikali yake katika kuleta miradi ya maendeleo inayochangia ustawi wa wananchi.









 


Post a Comment

0 Comments