TANGAZO

TANGAZO

MADAKTARI SITA WANUSURIKA AJALINI


Na Mwandishi Wetu, Mwanza


 Mwanza. Madaktari sita wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza  Sekou Toure wamepata ajali wakitokea kwenye kambi ya huduma ya matibabu Wilaya ya Kwimba mkoani humo.

Taarifa ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza iliyotolewa na Kamanda wa Polisi mkoani humo, Wilbrod Mutafungwa leo Jumamosi Machi 28, 2026 imesema ajali hiyo imetokea jana saa 12:30 jioni, katika barabara ya Jojiro, kitongoji na kijiji cha Maremve, Kata ya Igongwa, Wilaya ya Kwimba.

Kupitia taarifa hiyo, Mutafungwa amesema wakiwa kwenye gari namba T.231 AWT aina ya Toyota Land Cruiser Hardtop iliyokuwa ikiendeshwa na Dk James Nkya (38)  walipata ajali baada ya kujaribu kumkwepa mwendesha baiskeli.

"Madaktari hao walikuwa wanatoka kutoa huduma kwenye kambi ya matibabu ya kibingwa katika Hospitali ya Icheja, Wilaya ya Kwimba, wakiwa njiani kurudi Mwanza mjini,

"Walipofika kijiji cha Maremve, walipata ajali wakati dereva alipojaribu kumkwepa mpanda baiskeli aliyekuwa ameanguka barabarani

ndipo gari liliacha njia na kugonga gema la barabara, kisha kupinduka na kusababisha majeruhi kwa madaktari hao,"amesema Mutafungwa.

Amesema majeruhi katika ajali hiyo ni Dk James Nkya (38), Dk Self Mmka (38), Dk Stanley Makundi (37),  Dk Avetha Masawe (35), Dk Mary Urasa (27) na Dk Frank Mgeta (42).

"Majeruhi wanne bado wanaendelea na matibabu na majeruhi wawili wameruhusiwa baada ya hali zao kuimarika...chanzo cha ajali ni dereva wa gari kujaribu kumkwepa mpanda baiskeli aliyekuwa ameanguka katikati ya barabara hiyo ya vumbi,"ameeleza.

Jeshi la Polisi limeyataka makundi yote yanayotumia barabara kuendelea kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za matumizi sahihi ya barabara ili kuepuka ajali zinazoweza kuzuilika.

Maoni

Post a Comment

0 Comments