TANGAZO

TANGAZO

WACHIMBAJI TUNATAKA TUMILIKI DUBAI YETU, TUUZE MADINI YETU - RAIS BINA




Waziri wa madini Anthony Mavunde katikati, akiongoza maandamano ya amani ya wachimbaji wa madini mkoa wa Singida, kulia ni Rais wa shirikisho la vyama vya wachimbaji nchini John Bina na kushoto ni mkuu wa wilaya ya Iramba Suleiman Mwenda.

👉Asema amani iliyopo inufaishe sekta ya madini


👉Waziri Mavunde aeleza ujio wa viwanda vya kuongeza thamani madini hapa nchini 


👉Aitaja Kahama na uchakataji wa Nickel


Na Mwandishi wetu - Singida

Raisi wa shirikisho la vyama vya wachimbaji nchini, John Bina, ameishauri serikali kujenga soko la madini badala ya kuyasafirisha nje ya nchi.

Rais Bina ameyasema hayo leo Agosti 23, 2025, wakati wa kongamano la wachimbaji lililofanyika katika kijiji cha Nkonkilangi, kata ya Ntwike wilaya ya Iramba mkoani Singida.

Kongamano hilo lilikuwa na lengo la kumpongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, kutokana na kumpongeza Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa miaka minne ya mafanikio katika sekta ya madini.

Bina ametumia jukwaa hilo kuishauri serikali kujenga soko la madini badala ya kuendelea kusafirisha nje ya nchi, huku mapato makubwa yakinufaisha nchi hizo.

Amesema Tanzania ni nchi ya amani na hivyo itumike vyema kuleta manufaa kwa wananchi wake, sambamba na kuwapa fursa ya kunufaika na rasilimali za madini zilizopo kuanzia mwanzo hadi mwisho.

"Sisi kama wachimbaji tunaona kabisa ambavyo nchi yetu ina amani na utulivu, ni kimbilio la wageni wengi kutoka mataifa mbalimbali yenye vita, sasa tunataka Amani hii itupe faida" Amesema Bina

"Ni wakati sasa tupate Dubai yetu Tanzania, tunaomba soko la madini lipatikane hapa nchini, na ikiwezekana serikali iondoe kodi, tutaipata vinginevyo " Ameongeza

Amesema Tanzania kupitia wachimbaji wadogo, imejitambulisha duniani kote, na kuifanya shughuli hiyo kuwa rasmi tofauti na awali mtu akionekana mchimbaji anaonekana amekosa kazi za kufanya.

Katika hatua nyingine, Rais Bina ameongeza kuwa, wachimbaji wanakabiliwa na changamoto za mitaji ya kuendesha shughuli hiyo, hivyo kuiomba serikali kusimamia taasisi za kifedha ziweze kutoa mikopo ya masharti nafuu sambamba na kupunguza vikwazo vya utoaji wa mikopo hiyo.

Amesema ione namna ya kuongeza muda wa leseni za uchimbaji kutoka miaka 7 ya sasa hadi 25 ili waweze kukopesheka.

Nae mkuu wa mkoa wa Singida Halima Dendego amesema uchimbaji wa madini katika mkoa huo ni suala kuu la kiuchumi miongoni mwa mambo matatu yanayochochea uchumi wake ikiwemo kilimo na ufugaji.

Amesema sekta ya madini mkoani humo inakuwa kwa kasi huku kukishuhudiwa makusanyo makubwa ambapo kwa mwaka, mkoa umeweza kukusanya zaidi ya Shilingi bilioni 6.

Amesema serikali ya mkoa imejidhatiti kuunga mkono uendelezaji wa sekta ya madini ili kuendelea kuzalisha kwa tija kukuza uchumi wake na Taifa kwa ujumla.

Amesema "Sekta ya madini hapa Singida, tukizungumzia tu dhahabu, kwa mwaka tunaweza tukachinba na kuzalisha tani 2.7, lakini 1.5 inatoka kwa wachimbaji wadogo na tani 1.2 kwa mhodi mkubwa wa Shanta."

Kwa upande wake waziri wa madini Anthony Mavunde, amesema mafanikio makubwa yanayoshuhudiwa katika sekta ya madini ni asilimia 16 pekee ya Tanzania nzimaniliyofanyiwa utafiti.

Amesema serikali haina budi kuwekeza nguvu zaidi katika sekta hiyo, kwani maeneo mengi zaidi yakifikiwa sekta hiyo italeta manufaa makubwa kwa Taifa.

Amesema sambamba na hilo, serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, imedhamiria kujenga viwanda vya kuongeza thamani madini yanayozalishwa hapa nchini ili kuongeza ajira kwa wazawa pamoja na kuwainua wachimbaji wadogo.

Amesema kifungu cha 100 (D) cha sheria ya madini kinazuia usafirishaji wa madini nje ya nchi pasipo kuongezwa thamani.


"Hapa Tanzania hivi sasa tuna viwanda vinane vya kusafisha madini ya dhahabu, kuitoa kwenye jiwe la kawaida na kuipeleka kwenye usafi wa asilimia 99.9" Amesema Mavunde

Amesema wilayani Kahama mkoani Shinyanga, zimetengwa hekari 1,331 kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda cha kuongeza thamani madini ya Nickel yanayozalishwa mkoani Kagera.

Amesema pia vipo viwanda 9 vinajengwa vya kuongeza thamani madini mbalimbali kwenye maeneo mbalimbali nchini yakiwemo madini ya Shaba.


Kuhusu leseni ndogo za uchimbaji zinazotolewa


Waziri Mavunde amesema wadau wa sekta ya madini wanayo kila sababu ya kumpongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, kutokana na namna alivyoipendelea sekta hiyo ikiwemo utolewaji wa maeneo ya wachimbaji wadogo.

Amesema tangu ameingia kwenye wizara hiyo mpka sasa zaidi ya leseni 2,648 ambazo hazikuwa zinafanyiwa kazi zimefutwa na kurudishwa serikalini na maeneo hayo sasa yanagawanywa kwa wachimbaji wadogo.

Aidha ameonya wanaopata leseni ndogo za uchimbaji kuziuza, badala yake kila anayepata leseni ahakikishe anachimba kwa mujibu wa sheria na wala sio kupangisha.

Amesema endapo mwenye leseni ataingiza mtu amiliki duara kwenye leseni yake lazima azingatie mkataba wa makubaliano uliosajiliwa ofisi ya afisa madini katika mkoa husika.

"Moja ya changamoto kubwa nilizokutana nazo wizarani ni pamoja na migogoro mingi kati ya wenye maduara na wenye leseni, lakini Sheria haimtambui mwenye duara."

"Wachimbaji wengi wadodo mlihangaika sana. Sheria haimtambui mwenye duara, ni marufuku kwa atakayepewa leseni ndogo ya uchimbaji kupangisha watu, leseni ni ya kuchimba sio ya kuoangisha." Na kuongeza

Amesema kwa mwenye leseni anayetaka kupangisha ni lazima asaini mkataba kwa afisa madini ili atakapopata mwekezaji isitokee sintofahamu kati yake na mwenye duara.


Waziri wa madini Anthony Mavunde, akizungumza na wachimbaji wa mkoa wa Singida wakati wa kongamano la madini mkoani humo lililofanyika katika wilaya ya Iramba mkoani humo.


Rais wa shirikisho la vyama vya wachimbaji nchini John Bina, akizungumza na wachimbaji wa mkoa wa Singida wakati wa kongamano la wachimbaji lililolenga kumpongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kutokana kazi kubwa aliyoifanya katika kipindi cha miaka minne kwenye sekta ya madini nchini.



Mkuu wa mkoa wa Singida Halima Dendego akizungumza wakati wa kongamano la wachimbaji wa mkoa huo, lililolenga kumpongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa makubwa aliyoyafanya katika miaka minne ya uongozi wake kwenye sekta ya madini.











Post a Comment

0 Comments