TANGAZO

TANGAZO

SERIKALI INAENDELEA KUBORESHA MAZINGIRA YA KISERA, KUVUTIA WAWEKEZAJI NCHINI - DC NKINDA

 

Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mhe. Frank Nkinda na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa UTT AMIS, Prof. Faustine Kamuzora (kushoto) wakizungumza jambo ndani ya Kituo cha UTT AMIS - Kahama Mkoani Shinyanga



Na Mwandishi wetu, Kahama

Serikali ya Tanzania imesema itaendelea kuboresha mazingira ya kisera ili kuchochea shughuli za uwekezaji nchini, hususani katika masoko ya Mitaji na Fedha, katika kukuza uchumi na maendeleo ya wananchi.

Kauli hiyo ya serikali imetolewa jana jumatano Agosti 20, 2025 na mkuu wa wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga Frank Nkinda, wakati wa uzinduzi wa kampuni ya uwekezaji ya UTT AMIS wilayani humo.

Amesema lengo la ujio wa kituo hicho ni kuendelea kuwafikia wananchi wengi zaidi Mjini na Vijijini, kwa kuendelea kubuni na kutumia mifumo ya kisasa zaidi inayoruhusu utoaji wa huduma hizo za kifedha ikiwa ni pamoja na kukuza mitaji yao.

Amesema katika kuhakikisha huduma za kifedha zinamfikia kila mwananchi, Serikali inaendelea kufanya ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ikiwemo ya barabara, njia za mawasiliano na utengenezaji wa Sera stahiki ili kukuza uchumi wa wananchi wake.

Amesema “Napenda kuwahakikishia kwamba Serikali inafanya kila iwezalo kuhakikisha huduma za kifedha zinamfikia kila mtu kwa urahisi kabisa. Katika kuwahakikishieni hili, Serikali inaendelea kufanya uboreshaji wa miundombinu ili kukuza uchumi wa wananchi.”

Aidha ameutaka Mfuko wa Uwekezaji wa Pamoja wa UTT AMIS pamoja na wawekezaji wengine wilayani humo, kuhakikisha uwekezaji wao unakuwa na tija kwa wananchi wa Kahama, ikiwa ni pamoja na kutoa huduma za kipekee katika viwango vya kimataifa.


Nkinda ameisihi UTT AMIS kuwekeza katika utoaji wa huduma za kifedha kwa vijana waliopo maeneo ya migodini ambako kuna kundi kubwa la vijana huku wengi wao wakikosa elimu ya fedha.

Amesema “Niwaombe sasa katika mipango yenu mhakikishe elimu ya fedha inawafikia vijana waliopo migodini, kwani ni kundi kubwa lakini linakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa elimu ya fedha.”

Profesa Faustine Kamuzora, ni mwenyekiti wa bodi ya Uwekezaji ya UTT AMIS, amewashauri vijana kuwekeza kwenye mfuko huo ili wapate mtaji wa kujinyanyua kibiashara na kujikwamua na umasikini.

Profesa Kamuzora amesema vijana hawana budi kuwekeza kwani watu wengi wamekuwa masikini kwa kukosa elimu ya fedha hivyo wanapaswa kufanya kazi na kuwekeza ili kuondokana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza uzeeni.

"Mnaweza kuweka fedha kidogo kidogo hasa vijana, ili muweze kunufaika nguvu zinapoisha, kwani leo nyinyi ni vijana wenye nguvu lakini kesho mtakuwa mmezeeka na uwezo wa kufanya kazi utapungua, mkiwa na akiba hamtateseka.

Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Uwekezaji UTT AMIS Simon Migangala amesema walianza mwaka 2005 na asset ya shilingi bilioni moja na sasa ni miaka 20 wamefikia asset ya shilingi bilioni 20. Kila mwaka asset ilikuwa bilioni moja, na kwamba sababu za kukua kwao ni kujiamini na kuwepo uaminifu.

Amesema kwa kiasi kikubwa huduma inapatikana zaidi kwenye mitandao na wanaendelea kuiboresha kupitia tecknolojia na Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu imeonekana kukuza uwekezaji nchini.

Amesema "Tunipongeza serikali kwa kuendelea kutuwezesha mazingira mazuri ya uwekezaji na kuwa bora, kazi iliyobaki ni kuhudumia wananchi kuhakikisha wanawekeza na kupata faida kwa wakazi wa Kahama na Mikoa ya jirani"

Baadhi ya wakazi wa Kahama akiwemo Ester Kimaro na Yohana Ntemi wameishukuru serikali kwa kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji wilayani humo.


“Ni jambo zuri ila tunaiomba serikali ione namna wananchi watanufaika moja kwa moja na wawekezaji, kwa kuanza kufaidika wawe ni wananchi wa chini itasaidia kuleta maana halisi ya uwekezaji.”amesema Kimaro

Nae Yohana Ntemi amesema tatizo lililopo vijana hawana elimu ya maswala ya kutunza fedha,ambapo ameomba elimu hiyo kuwafikia vijana wengi ili waweze kuwekeza na kuongeza mitaji yao.


Kampuni ya Uwekezaji ya UTT Asset Management and Investor Services (UTT AMIS) imezindua tawi jipya mjini Kahama mkoani Shinyanga, hatua inayolenga kusogeza karibu huduma za kifedha na uwekezaji kwa wananchi katika maeneo ya kiuchumi ikiwemo migodini.



Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mhe. Frank Nkinda na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa UTT AMIS, Prof. Faustine Kamuzora (kulia) wakikata utepe ishara ya uzinduzi wa Tawi la UTT AMIS - Kahama Mkoani Shinyanga Agosti 20,2025.

(NB- Picha zote na Kadama Malunde)




Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mhe. Frank Nkinda akionesha nyaraka baada ya kufungua akaunti wakati wa uzinduzi wa Tawi la UTT AMIS - Kahama Mkoani Shinyanga




Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa UTT AMIS, Prof. Faustine Kamuzora akizungumza wakati wa uzinduzi wa Tawi la UTT AMIS - Kahama Mkoani Shinyanga




Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mhe. Frank Nkinda akizungumza wakati wa uzinduzi wa Tawi la UTT AMIS - Kahama Mkoani Shinyanga







Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa UTT AMIS, Prof. Faustine Kamuzora akizungumza wakati wa uzinduzi wa Tawi la UTT AMIS - Kahama Mkoani Shinyanga



Mkurugenzi Mtendaji wa UTT AMIS, Simon Migangala, akizungumza wakati wa uzinduzi wa Tawi la UTT AMIS - Kahama Mkoani Shinyanga






























Post a Comment

0 Comments