TANGAZO

TANGAZO

Zaidi ya Sh Bilioni 1.14 kutumika maandalizi ya kuupanga Mji wa Kahama kidigitali

 


Mratibu wa TACTIC kutoka Urban Solution – Dar es Salaam, Elias Nyabusani akizungumza kwenye mkutano na wakuu wa idara wa Halmashauri ya Manispaa ya Kahama pamoja na taasisi zinazotoa huduma ndani ya Manispaa hiyo, kwa lengo la kujadili mpango kabambe wa kidigitali wa Manispaa ya Kahama.


Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga ni moja ya Manispaa zinazokabiliwa na changamoto ya makazi holela, yanayochangia kuwepo kwa migogoro sugu ya ardhi, maafa ya mafuriko, hali inayoisukuma serikali kuja na mpango huo uliopo chini ya mradi wa uboreshaji Miji ya Tanzania (TACTIC).


Kutokana na changamoto hizo, Zaidi ya Sh bilioni 1.14 zinatarajiwa kutumika katika maandalizi ya mpango kabambe wa kidigitali (Master Plan), wa Halmashauri ya Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga, utakaodhibiti makazi holela yanayochangia maafa ikiwemo mafuriko kipindi cha mvua.


Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama, Robert Kwela, amesema Kahama ni miongoni mwa Miji inayokuwa kwa kasi kutokana na wimbi kubwa la watu wanaoingia kwa ajili ya kufanya shughuli za kibinadamu, hali inayosababisha miundonbinu iliyopo kuzidiwa na idadi ya watu na shughuli za kibinaadam.


Kwela ameyasema hayo wakati wa mkutano wa wadau ambao ni wakuu wa idara pamoja na taasisi zinazotoa huduma ndani ya Manispaa hiyo, kujadili mpango kabambe wa kidigitali wa upangaji mji wa Kahama.


Amesema kutokana na changamoto ya mipango Miji, kumekuwa na ucheleweshwaji wa ukamilishaji wa miradi inayotekelezwa chini ya Tactic hususani katika kipengele cha miundombinu a barabara, kwani maeneo mengine mkandarasi akiwa anaendele na shughuli zake anakutana na miundombinu ya umeme, mabomba ya maji au waya za TTCL hali inayochelewesha huduma kwa wananchi.


Amesema " Tunashuhudia leo tumepitia changamoto kubwa kwenye utekelezaji wa miradi ya Tactic kwenye eneo la miundombinu, kuna mahali ambapo barabara inapita mkandarasi anakutana na nyaya za TTCL, mabomba ya maji, waya za Tanesco, lakini mfumo huu utahakikisha mifumo inasomana kuondoa changamoto hizo "


Amesema wamejipanga kuwafikia wananchi katika makundi mbalimbali kuwaelimisha na kuwapa taarifa kuhusu ujio wa mradi huu kwenye mitaa na vijiji vyao kupitia mikutano ya hadhara na wataalamu watakaofika kwenye maeneo yao, wawapokee.


Ameongeza kuwa manispaa hiyo ina jumla ya mitaa 32 na vijiji 45, na matarajio ni kuwa baada ya utekelezaji wa mpango huu, maeneo yote yatapangwa rasmi kama mitaa, hivyo kuondoa mfumo wa vijiji.


Amesema mradi huo wa kutayarisha mpango kabambe utagharimu zaidi ya shilingi Bilioni 1.14, kwa hiyo wao kama Manispaa wanao wajibu wa kuutekeleza kwa ufanisi mkubwa ili uwe na manufaa chanya kwa wananchi.


Mratibu wa Tactic kutoka Urban Solution - Dar es Salaam Elias Nyabusani, amesema lengo la mradi huo ni kuondoa makazi holela Kahama, kudhibiti ufanyaji holela wa shughuli za kibinadamu ili kuuwezesha mji kukua katika mpangilio unaostahili na kuwa miongoni mwa Miji itakayokuwa imefanikiwa kudhibiti makazi holela.


Amesema "Hata sasa ukiangalia namna shughuli zinavyotekelezwa katika Mji huu, hakuna utaratibu unaoeleweka, utakuta barabara zimegeuzwa kuwa maduka, sehemu zinazojaa maji wakati wa mvua zimejengwa, mifereji imeziba"


Na kuongeza"Mradi utakapokamilika na ukatekelezwa, utachanganua miundombinu iliyopo itakavyohimili watu waliopo na huduma zitakazokuwa zinafanyika. Kwa hiyo tunaondoa changamoto za makazi, barabara, maji ya mvua, miundombinu ya maji taka na kama ni viwanda viwe sehemu yake, makazi yawe sehemu yake"


Amesema mpango huo kabambe unakwenda kutengenezwa kwa mfumo wa kidigitali ambao haujawahi kutekelezwa katika Manispaa yoyote nchini na Kahama imekuwa ya kwanza kuupata mpango huo.


Amewatoa hofu wakazi wa Kahama kuwa mradi huo hautawanyang'anya ardhi zao, bali ikitokea inahitajika taratibu zote zitafuatwa na kwamba mradi huu una faida kubwa kwao.


Baadhi ya wadau wa mradi huo kutoka taasisi mbalimbali zinazotoa huduma ndani ya Manispaa ya Kahama wamesema mpango huo utawasaidi katika utekelezaji wa shughuli zao kwa wananchi.


Wadau hao akiwemo Anna John, kutoka wakala wa huduma za misiti Tanzania (TFS) wilaya ya Kahama amesema mradi huo utasaidia kuondoa migogoro kati yao na wananchi kwani wataijua mipaka yao na ya hifadhi.


Amesema "Mradi huu utasaidia sana kuondoa migogoro ya mipaka kati ya maeneo ya hifadhi ya misitu na vijiji, kwani kila upande utakuwa na uelewa wa mipaka yake kwa ustawi wa uhitadhi wetu "


Naye Fred Mwamoto ambaye ni ofisa mkuu wa usimamizi wa ushuru kutoka mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) mkoa wa kikodi Kahama, amesema

"Katika taasisi yangu mpango huu unapofanyika pengine ukahitaji baadhi ya vitu viweze kufanyika kwa kodi au msahama wa kodi, kwa hiyo tuko tayari kutoa ushirikiano pale yanapohitajika hayo. Utatusaidia kuwafikia wateja wetu kiurahisi na hakuna anayekwepa kodi kwani Mji ukiwa na mpangilio ni rahisi kujua kila mteja alipo"


Maoni ya wananchi

Baadhi ya wakazi wa Kahama akiwemo Maria Ndimbo mkazi wa kata ya Majengo akizungumzia mradi huo ameiomba serikali kuuharakisha ili wananchi haswa wa Majengo waondokane na adha ya mafuriko inayotokana na maji ya mvua yanayokosa uelekeo kutokana na kutokuwa na mitaro ya maji ya mvua hali inayotokana na mpangilio mbovu wa Mji.


Amesema "Sisi tunaupokea kwa mikono miwili, lakini je utafanikiwa au ni maneno tu? Maana sisi wa huku tunateswa na mafuriko kipindi cha mvua kwa sababu hakuna mitaro ya kupokea haya maji, badala yake yanajaa kwenye nyumba zetu, kwa hiyo kama ni kweli tutashukuru sana"


Nae Juma Mwandu mkazi wa kata ya Mhongolo, Kahama ameipongeza na kushukuru serikali kwa mpango huo kabambe, aliosema utakuwa mkombozi wa changamoto wanazopitia hususani katika miundombinu ya barabara.


" Mimi nawapongeza sana serikali kwa hatua hii, tumefurahi na kufarijika mno. Huenda huu mpango ukawa neema kwetu kwa sababu barabara hazieleweki, hapa tunawaza ikitokea janga la moto hata hao zimamoto watapita wapi? Yote hii ni kwa sababu hakuna mpangilio wa mji, hata barabara za mitaa zilizopo zinashindikana kutengenezwa, matokeo yake mvua zikinyesha hizi barabara ndo zinakuwa mitaro ya maji"


Halmashauri ya Manispaa ya Kahama imekuwa Manispaa ya kwanza nchini kufikiwa na mpango huo wa miaka 25, kutokana na hali ya miundombinu iliyopo kushindwa kuendana na kasi ya ongezeko kubwa la watu, jambo ambalo limeonekana kukwamisha maendeleo na ukuaji wa Mji.




Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama Robert Kwela, akizungumza na wanahabari baada ya kumalizika kwa mkutano huo.





Mwisho.

Post a Comment

0 Comments