TANGAZO

TANGAZO

"VYAMA VYA SIASA MARUFUKU KUINGILIA ZOEZI LA UBORESHAJI" - INEC

Makamu Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) Jaji Mstaafu Mahakama ya Rufaa Mbarouk Salim Mbarouk ,akizungumza leo Septemba 13,2024 jijini Dodoma wakati akifungua Mkutano wa Tume na wadau wa uchaguzi mkoani Dodoma.
Mwalikishi wa Mkurugenzi wa Uchaguzi Seleman Mtibora akizungumza kwenye mkutano wa Tume hiyo na wadau wa Uchaguzi kuhusu uboreshaji wa Daftari la kudumu la wapiga kura leo September 13,2024 Jijini Dodoma

Na Okuly Julius, Dodoma


Makamu Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) Jaji Mstaafu Mahakama ya Rufaa Mbarouk Salim Mbarouk , amewataka wadau wa Uchaguzi Mkoani Dodoma kutumia nafasi zao kutoe elimu kwa wananchi kuhusu utaratibu wa kujiandikisha na kuboresha taarifa zao katika Daftari la kudumu la wapiga kura.

Akizungumza leo Septemba 13,2024 jijini Dodoma wakati akifungua Mkutano wa Tume na wadau wa uchaguzi mkoani humo, Jaji Mstaafu Mbarouk, amesema suala la kujiandikisha kuwa Mpiga Kura zaidi ya mara moja ni kosa la kisheria kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 114(1) cha Sheria ya Uchaguzi.

Ambao amesema Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na.1 ya mwaka 2024, kifungu hicho kinasema kuwa, mtu yeyote atakayeomba kuandikishwa zaidi ya mara moja atakuwa ametenda kosa la kisheria na akitiwa hatiani adhabu yake ni faini isiyopungua kiasi cha shilingi laki moja na isiyozidi laki tatu au Kutumikia kifungo kwa kipindi kisichopungua miezi sita na kisichozidi miaka miwili au vyote kwa pamoja.

"Nitoe rai kwenu kama wadau wa uchaguzi,mkawaelimishe wananchi wanaokwenda vituoni kwa ajili ya kuomba kuandikishwa kuwa wapiga kura, kuomba kuandikishwa kuwa wapiga kura mara moja tu ili kuepuka uvunjaji wa Sheria,"ameeleza Jaji Mstaafu Mbarouk

Katika hatua nyingine Jaji Mstaafu Mbarouk, amesema kuwa Kila Chama cha Siasa kimepewa nakala ya orodha ya vituo vyote vya kuandikisha wapiga kura, hivyo nakala hizo zitawasaidia kupanga na kuweka mawakala wa uandikishaji katika vituo vya kuandikisha wapiga kura.

"Kila Chama kitaruhusiwa kuweka Wakala mmoja kwenye kituo cha kuandikisha wapiga kura kwa lengo la kushuhudia utekelezaji wa zoezi la uboreshaji kituoni ikiwemo kuwatambua wale wanaokuja kituoni kama wana sifa za kuandikishwa,"

Na kuongeza kuwa "Mawakala au viongozi wa vyama vya siasa hawaruhusiwi kuingilia mchakato wa Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la wapiga kura kituoni," amesema Jaji Mstaafu Mbarouk

Kwa upande wake Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Tume Huru ya Taifa ya uchaguzi (INEC) Bw. Selemani Mtibora amesema kwa mkoa wa Dodoma kuna vituo 2,721 vitakavyotumika kwenye uboreshaji kwa nwaka huu ikiwa ni ongezeko la vituo 37 katika vituo 2,684 vilivyotumika kwenye uboreshaji mwaka 2019/20.

Mtibora ameongeza kuwa jumla ya wapiga kura 594,494 wanatarajiwa kushiriki zoezi hilo ambapo watakao kosa sifa wataondolewa kwenye daftari la kudumu la wapiga kura.

"Hivyo, baada ya uboreshaji inatarajiwa kuwa daftari litakuwa na jumla ya wapiga kura 34,746,638 pia idadi hii inaweza kuongezeka kwa kuwq inawezekana wapo watanzania ambao walikuwa walikuwa na sifa za kuandikishwa kuwa wapiga kura wakati wa daftari la uboreshaji mwaka 2019/20 lakini kwasababu moja au nyingine hawakuweza kujiandikisha kuwa wapiga kura," amesema.

Naye Mratibu wa Uandikishaji Mkoa wa Dodoma Bw. Charles Mduma, amesema zoezi hilo litafanyika katika Halmashauri nne ambazo ni, Kongwa,Chamwino,Dodoma Mjini na Bahi ambapo tayari wameshaanza mafunzo kwa wadau ambayo itafanyika kuanzia ngazi ya Mkoa mpaka Jimbo na tayari watendaji wote watakaosimamia zoezi wameshapatiwa miongozo.

"niwaase wanasiasa kuzingatia miongozo na taratibu zilizotolewa na Tume ili kufanya zoezi hili kuwa la haraka na kusiwepo na changamoto yeyote kwa kifupi kila mmoja atimize wajibu wake," amesema Mduma

Mzunguko wa Tano wa Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura utajumuisha Mikoa ya Dodoma, Singida na Manyara, ambapo Mkoa wa Dodoma ni katika Halmashauri nne ya Kongwa,Chamwino,Dodoma Mjini na Bahi, huku Mkoa wa Manyara ni katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu na Wilaya ya Kiteto na Simanjiro, kuanzia tarehe 25 Septemba hadi tarehe 1 Oktoba 2024 na vituo vitafunguliwa kuanzia saa mbili asubuhi na Kufungwa saa kumi na mbili jioni.

Kwa Mujibu wa Kifungu cha 168 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na.1 ya Mwaka 2024 kadi za Mpiga Kura zilizotolewa mwaka 2015 na 2020 zenye jina la TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI ni halali na zitaendelea kutumika kwenye chaguzi zijazo, hivyo zoezi hili la uboreshaji wa Daftari haliwahusu wapiga Kura wenye kadi hizo.





Baadhi ya wadau wa Uchaguzi walioshiriki mkutano wa wa Tume na wadau wa wa uchaguzi kuhusu uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura leo September 13,2024 kwenye ukumbi wa Tume hiyo Jijini Dodoma

Post a Comment

0 Comments