Picha ya pamoja ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi EWURA, Prof. Mark Mwandosya (waliokaa katikati) na wajumbe wa Kamati ya Tathmini ya Utendaji, Usimamizi na Matokeo ya udhibiti wa huduma za umeme kutoka nchi za Uganda, Namibia, Afrika Kusini, Ghana na Kenya, baada ya kikao kilichofanyika tarehe 9 jijini Dar es Salaam. Tathmini hiyo inaratibiwa na Chuo Kikuu cha Cape Town cha Afrika Kusini.
Na.Mwandishi Wetu.
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imeanza kufanyiwa tathmini ya utendaji, usimamizi na udhibiti wake katika sekta ya umeme nchini.
Tathmini hiyo inayoratibiwa na Chuo Kikuu cha Cape Town cha nchini Afrika Kusini, itafanyika kwa siku tano (Septemba 9 hadi 14, 2024,) na inafanywa na wajumbe ambao ni watendaji wakuu wa taasisi za udhibiti kutoka nchi za Uganda, Namibia, Afrika Kusini, Ghana na Kenya .
Mapitio hayo hulenga kutathmini utoshelevu wa udhibiti, nyenzo za udhibiti na athari zake katika utendaji wa sekta ya umeme na hivyo kukuza mbinu bora za kiudhibiti kwa ajili ya kuboresha utoaji wa huduma za umeme katika nchi husika.
Pamoja na mambo mengine wajumbe wa kamati ya tathmini watakutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati nchini, Dkt Doto Mashaka Biteko (Mb), Bodi ya EWURA chini ya Mwenyekiti wake, Prof Mark Mwandosya, Menejimenti ya EWURA, Shirika la Umeme (TANESCO), wazalishaji na watoa huduma za umeme binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali ( NGOs), sekta binafsi, mashirika ya kijamii yanayojihusisha na masuala ya umeme na watendaji wa vyombo vya habari nchini ili kujadiliana nao na kupokea maoni yao kuhusu huduma za umeme.
Tathmini ya EWURA ni ya sita (6) kufanyika kwa taasisi za udhibiti ikiwa imetanguliwa na Mamlaka ya Taifa ya Udhibiti wa Nishati ya Afrika Kusini (NERSA), Mamlaka ya Udhibiti Nishati ya Kenya (ERA), Mamlaka ya Udhibiti ya Uganda (ERA), Bodi ya Udhibiti Umeme ya Namibia ( ERB) na Mamlaka ya Udhibiti Huduma za Nishati ya Ghana(PURC). Tanzania ilishiriki katika mchakato wa mapitio hayo kwa mara ya mwisho mwaka 2010.
Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dkt James Andilile(kulia) akiwakaribisha Wakuu wa Taasisi na Wataalam waliohudhuria kikao cha Tathmini ya Utendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kwenye sekta ya umeme, iliyoanza leo tarehe 9 Septemba 2024.
Kikao cha mapitio ya tathmini ya utendaji wa EWURA katika sekta ya umeme kikiendelea leo 9 Septemba 2024 katika ofisi za EWURA Kanda ya Mashariki, jijini Dar es Salaam
Picha ya pamoja ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi EWURA, Prof. Mark Mwandosya (waliokaa katikati) na wajumbe wa Kamati ya Tathmini ya Utendaji, Usimamizi na Matokeo ya udhibiti wa huduma za umeme kutoka nchi za Uganda, Namibia, Afrika Kusini, Ghana na Kenya, baada ya kikao kilichofanyika tarehe 9 jijini Dar es Salaam. Tathmini hiyo inaratibiwa na Chuo Kikuu cha Cape Town cha Afrika Kusini.
Picha ya pamoja ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi EWURA, Prof Mark Mwandosya (waliokaa katikati), wajumbe wa Bodi ya EWURA, Menejimenti na wajumbe wa Kamati ya Tathmini ya Utendaji, usimamizi na matokeo ya udhibiti wa huduma za umeme kutoka nchi za Uganda, Namibia, Afrika Kusini, Ghana na Kenya, baada ya kikao kilichofanyika tarehe 9 Septemba 2024 jijini Dar es Salaam. Tathmini hiyo inaratibiwa na Chuo Kikuu cha Cape Town cha Afrika Kusini.
0 Comments