Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt John Jingu amewataka watumishi wa afya kuwatengenezea fikra njema wananchi katika kukabiliana na magonjwa mbalimbali hasa magonjwa ya mlipuko ikiwemo ugonjwa wa Kipindupindu.
Dkt. Jingu ameyasema hayo leo Machi 25, 2024 wakati akipokea taarifa ya sekta ya afya Mkoa wa Mwanza iliyowasilishwa na Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Thomas Rutachunzibwa kuelezea hali ya huduma za afya katika mkoa huo.
Dkt. Jingu amesema ili kukabiliana na magonjwa ya mlipuko silaha kubwa ni kubadilisha fikra za wananchi kwa kuwajengea uwezo wa namna ya kukabiliana na magonjwa hayo ikiwemo ugonjwa wa Kipindupindu ambao umekuwepo katika mkoa huo.
Aidha, Dkt Jingu amewataka watumishi hao kuzingatia ubora wa huduma za afya kwa wananchi kwa kuzingatia staha, utu na heshima na kuzitoa kwa ubora wake kwani serikali imeweka miundombinu rafiki kwa ajili ya kutolea huduma za afya nchini.
"Tuna jukumu kubwa katika kutoa huduma bora za afya, tunao uwezo wa kuhakikisha tunatelekeza huduma hizo, niwasisitize na kuwaomba kuzingatia ubora wa huduma kwa wananchi, naamini kwa uwezo tulionao tuendelee kuimarisha miundombinu tuliyonayo katika kuboresha huduma za afya kwa wananchi"
Aidha Dkt. Jingu amesema Serikali itaendelea kutimiza majukumu yake ikiwemo upatikanaji wa dawa, uboreshwaji wa miundombinu huku akiwataka kuiendeleza miundombinu iliyopo kuendelea kuboresha huduma za afya.
Awali akiwasilisha taarifa Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt Thomas Rutachunzibwa amesema kuwa Mkoa wa Mwanza umeendelea kukabiliana na ugonjwa wa Kipindupindu katika maeneo mbalimbali kwa kutoa elimu juu ya namna bora ya kujikinga pamoja na kugawa dawa ya kutibu maji ili wananchi watumie maji safi na salama.
0 Comments