Na Mwandishi Wetu
KILIMANJARO - Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Jumanne Sagini (Mb) amewataka Wananchi Wilayani Hai Mkoani Kilimanjaro kuacha kujihusisha na dawa za kulevya aina ya mirungi na bhangi ili kuepuka kuwa wateja wa Jeshi la Polisi na hatimaye kuishia Magerezani.
Mhe. Sagini alibainisha hayo Machi 20, 2024 wakati akiwasalimia Wananchi wa Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro kwenye Mkutano wa hadhara wa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango aliyepo Mkoani humo kwa ziara ya kikazi.
"Mhe. Makamu wa Rais hatuna matukio makubwa ya uvunjifu wa amani maeneo haya, isipokuwa matukio madogo madogo ya kujirudia ikiwemo utumiaji wa dawa za kulevya aina ya mirungi na bhangi hivyo niwatake Wananchi kuachana na utumiaji wa dawa hizo ili kuepuka kusumbuliwa na Jeshi letu la Polisi na Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya pia kumekuwepo na mgogoro wa wakulima na wafugaji katika kipindi cha kiangazi hivyo nitoe rai kwenye kamati zetu za Usalama za Wilaya na Mkoa kutenga maeneo na kuimarisha mahusiano mema kati ya wakulima na wafugaji" Alisema Sagini.
Pia Mhe. Sagini alimpongeza Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa ajira katika sekta zote za Usalama wa Raia na Mali zao kwani Askari 4000, wanatarajiwa kuongezwa mwaka huu na pia kuwapandisha vyeo Askari wa vyeo mbalimbali, Wakaguzi, Maafisa wa ngazi ya chini na Maafisa Wakuu zaidi ya 35000 kwa mara moja ambapo haijawahi kutokea hapo awali tangu nchi ipate Uhuru.
Aidha, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Jeshi la Polisi Mkoani Kilimanjaro kwa kushirikiana na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya "DCEA" ilifanya Operesheni Juni 2023 hadi Februari 2024, ambapo waliteketeza ekari 535 za mashamba ya Dawa za Kulevya aina ya Mirungi Wilayani Same, Kukamata kilogramu 71.1795 za Mirungi na gramu 0.2 za Heroin katika Operesheni za kutokomeza vijiwe vya matumizi ya dawa za kulevya zilizofanyika Moshi Mjini na Kukamata gramu 1998 za bhangi Wilayani Rombo.
0 Comments