Na Mapuli Kitina Misalaba
Katibu wa SMAUJATA Kanda ya Ziwa, Daniel Kapaya, ameanza ziara yake mkoani Geita, ambapo leo amefika katika Ofisi ya Polisi Mkoa wa Geita na kupokelewa na ACP Mimata, Mkuu wa Operesheni wa Mkoa wa Geita, pamoja na SSP Thomas Mtikatika, Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Geita, kwa niaba ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, ACP Sofia Jongo.
Uongozi wa jeshi la polisi unathibitisha mchango mkubwa wa SMAUJATA katika kuibua na kupinga vitendo vya ukatili kwenye jamii, zikiwemo mimba za utotoni, ulawiti, ubakaji, ukeketaji, na ajira za watoto.
ACP Mimata anasema SMAUJATA imekuwa msaada mkubwa katika kufichua vitendo vya kihalifu na kuimarisha ulinzi wa haki za watoto na wanawake.
Kwa upande wake, Daniel Kapaya ameliomba jeshi la polisi kuendelea kushirikiana na mashujaa wa SMAUJATA katika utekelezaji wa majukumu yao.
Amesisitiza kuwa mashujaa wanahitaji msaada wa usafiri na kushirikishwa kwenye vikao au kampeni yoyote inayohusiana na kupinga ukatili ili waweze kutoa elimu kwa jamii kwa ufanisi zaidi.
Kapaya pia amewaelekeza viongozi wa SMAUJATA katika ngazi zote kuanzia vitongoji hadi mkoa kuendelea kufikia maeneo tofauti kwa lengo la kutoa elimu ya kupinga ukatili bila kujali ukabila, dini, ukanda au itikadi za kisiasa.
Amesisitiza kuwa ni muhimu viongozi wasioonyesha ushirikiano kuchukuliwa hatua za kupunguzwa mamlaka ili kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa majukumu ya SMAUJATA.
Katibu wa SMAUJATA Mkoa wa Geita, Bw. Frank Kapiligi, amemshukuru Katibu wa Kanda ya Ziwa kwa kufanya ziara katika Mkoa wa Geita na kuweza kujenga uwezo mkubwa wa kiutendaji. Kapiligi anasema Geita imepokea maelekezo yote yaliyotolewa na Katibu wa Kanda ya Ziwa na inaahidi kuyatekeleza kwa ufanisi.
Ziara hii inaendelea kuboresha ushirikiano kati ya SMAUJATA na jeshi la polisi kwa lengo la kutokomeza vitendo vya ukatili katika jamii.

0 Comments